Thursday 10 December 2015

Wataalamu wa Afya washauri jamii ijenga tabia ya Ulaji wa Chakula bora


MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Sokoine Sua cha Mjini Morogoro ambaye ni Mtaalamu wa Chakula na Lishe, Prof. Joyce Kinabo, amesema idadi kubwa ya wananchi nchini bado wanauelewa mdogo wa masuala ya chakula na lishe, hivyo kupelekea watu wengi kuugua magonjwa yatokanayo na ukosefu wa baadhi ya madini mwili.

Aidha, imeelezwa kwamba lishe bora ni kichocheo cha ustawi bora wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na siasa juhudi za kuinua kiwango cha lishe kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa zinahitajika.

Professa Kinabo amenunuliwa na FikraPevu akisema, kuishi vizuri ni pamoja na kula chakula bora na sahihi. Pia, amesema mtu anayeishi vizuri ni yule ambaye hasumbuliwi na maradhi hatari na njia pekee ya kuulinda mwili dhidi ya maradhi hatari ni kujua ipasavyo na kuvitumia vyakula bora pamoja na kufanya mazoezi.

Katika kuliwekea msisitizo jambo hilo, Prof. Kinabo ameeleza kuwa baadhi ya wataalamu wa malezi na afya wanayo miongozo maalumu inayowawezesha wazazi kuzingatia afya ya familia zao kwa kujenga utaratibu wa kula chakula bora
.
“Tumekuwa tukiona watoto wetu wakipenda kula vyakula kutokana na utamu wake, huku wakiwa hawajali kabisa kiwango cha virutubisho kilichomo kwenye chakula husika. Jambo hili linaleta changamoto nyingi hasa linapokuja suala la kusisitiza ulaji wa vyakula fulani fulani ili kujenga afya zao” alieleza.

Aidha, ameeleza kuwa hata kama ni vigumu kuwahamasisha watoto wa miaka minane kula matunda badala ya biskuti ni vyema wakazoeshwa kula matunda kwani bila hivyo itakuwa ni mtihani mkubwa atakapokuwa mkubwa.

“Jambo hili mara kadhaa linasababisha matatizo kadha wa kadha kiafya ikiwa ni pamoja na tatizo la uono hafifu au upungufu wa damu. (Yote haya tiba yake ni ulaji wa matunda na mbogamboga)” alifafanua.

Amezitaka taasisi na mamlaka zinazohusika kuboresha usalama wa chakula na ulinzi kwa walaji na kuitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), pamoja na Shirika la Viwango nchini (TBS), kuhakikisha usimamizi bora wa bidhaa zinazoingia nchini kwa kupitia maeneo husika zinapatikana kwa ajili ya matumizi ya binadamu sambamba na kuwa na ubora.

Wataka tafiti za wataalamu zitumike 
Kwa upande wake Mhandishi wa Chakula kutoka Chuo cha Sokoine Sua, Prof. Bernard Chove, ametaka Serikali kutumia tafiti zinazotolewa na wataalamu nchini na kuzifanyia kazi, sambamba na taasisi hizo kutoa elimu ya kutosha kuhusu vyakula.

Amesema kwamba lishe bora ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi kwa kila taifa na kwamba kwamba kuwekeza kwenye lishe ni muhimu ili kupunguza umaskini kwa kuhakikisha kila mwanajamii anachangia kwa taifa lake.

“Inabidi walaji waelimishwe kwasababu kama mtu hajui maji ya moto ninini, haisaidii na mlaji naye anapoambiwa nawa ule lakini haelewi maana yake kuwa ninini, anaweza kusema amenawa kumbe kaloweka mikono kwenye maji, taarifa hizi kwa nchi yetu ni chache sana, hatuwezi kujigamba kwamba tuna taarifa sahihi" alifafanua na kuongeza Prof. Chove.

Elimu ya lishe
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, kutokana na utamaduni wa kutozingatia lishe bora na vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili, matatizo ya udumavu, utapiamlo na ukondefu yamekua yakiwapata watoto wengi nchini kuliko watu wazima.

Tatizo kubwa linaelezwa kwamba ni uelewa wa watu juu ya mahusiano kati ya lishe na maendeleo ya mtoto kitaaluma, kipimo kikubwa kinachotumia kupima hali ya udumavu ni watoto wenye umri kati ya miaka 0 mpaka 5, (0-5). Katika umri huo mtoto asipopata lishe na virutubisho muhimu anaweza kupata udumavu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, badala ya kujaza keki, biskuti na ice-cream, majumbani, mara kadhaa wazazi wametakiwa kuhakikisha wanaweka karoti, embe, ndizi na matunda mengine ili kuwasaidia watoto kula, pale wanaposikia hamu ya kula.

Pia kwa muda mrefu Tanzania imeendelea kuunga mkono jitihada za kitaifa na kimataifa katika kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na lishe bora yenye virutubisho muhimu inapatikana kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, mwaka 2013 Serikali ilizindua Program ya Kitaifa ya Uboreshaji wa Chakula ambapo virutubisho muhimu viliongezwa kwenye vyakula vinavyoliwa zaidi katika jamiii ya Watanzania ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 25 ya watu wanatumia unga wa ngano na mahindi pamoja na mafuta ya kupikia yaliyoongezwa virutubisho vyenye madini na vitamin muhimu kama chuma, zinki na Vitamini A na B12.

Mkakati wa Lishe wa Kanda ya Afrika kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015-2025 uliozinduliwa mwezi Julai mwaka huu, ulisisitiza ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika kuboresha lishe ikiwemo sekta binafsi.

Chanzo; fikrapevu

No comments:

Post a Comment