Tuesday 12 April 2016

APOTEZA KICHANGA WODINI


Na Gordon Kalulunga, Mbeya

MTOTO mchanga wa siku nne amefariki dunia katika Hospitali teule ya wilaya ya Mbeya, Ifisi Mbalizi kwa kile mzazi wake alichodai kuwa ni kutopata msaada kutoka kwa wauguzi wa Hospitali hiyo.

Tukio hilo limetokea usiku wa saa sita Machi 27, mwaka huu ndani ya wodi ya wazazi hospitalini hapo.

Akizungumza na Gazeti hili nyumbani kwao baada ya mazishi ya kichanga hicho, mama mzazi wa mtoto huyo Paulina Daud (22), huku akilia alisema kuwa, alipelekwa Hospitalini hapo akiwa mjamzito Machi 24, mwaka huu, majira ya saa tatu asubuhi ambapo saa tano alijifungua kwa njia ya upasuaji.

“Mtoto alikuwa salama na alikuwa akinyonya vizuri nami nikiwa naendelea kuuguza kidonda mpaka tarehe 26 usiku wa saa nne mtoto akawa analia sana ndipo nikaomba msaada kwa muuguzi mmoja akasema yeye hausiki na wodi letu” alisema Paulina.

Alisema pamoja na maumivu ya kidonda chenye mshono, alipoona mtoto anazidi kulia akaamua kujikongoja mpaka chumba cha wauguzi na kuwaeleza tatizo lake, badala ya kwenda kumsaidia wakamwambia aende akamchukue mwanae na kumpeleka chumba walichokuwa wauguzi.

“Nikarudi wodini na kumbeba mtoto kwa shida kisha kumpeleka chumba cha wauguzi na mmoja wa wauguzi akasema nimwamshe mwenzake aliyekuwa amelala pembeni na nilipomwamsha wakamwangalia mwanangu wakasema tayari amefariki” alisema Paulina huku akiangua kilio…

Mama mzazi wa Paulina Sekela Daud, alisema kichanga tangu kipate uhai wake hakikuwa na matatizo yeyote na kwamba, alipopata taarifa ya kifo hicho alishtuka na kuamua kutafuta usafiri kutoka Mbalizi usiku huo na kwenda Hospitalini.

“Nilifika saa kumi na moja alfajiri Hospitalini na niliwaomba walinzi waniruhusu kwa kuwaambia kuwa nilikuwa nimeitwa na wauguzi kwa tatizo la mwanangu, wakaniruhusu na nilipofika nikakuta hali hiyo na nilipowauliza wakasema hawajui sababu yeyote iliyosababisha kifo cha mjukuu wangu” alisema Sekela.

Alisema baada ya taratibu na mabishano kadhaa hospitalini hapo, wakaruhusiwa kutoka na maiti majira ya saa tatu asubuhi na mama mzazi wa kichanga aliruhusiwa kutoka majira ya saa sita mchana na anatakuwa kwenda Hospitalini hapo kutoa nyuzi April 5, mwaka huu.

Machi 29, mwaka huu, mwandishi wa habari hii alifika katika Hospitali hiyo ya Ifisi Mbalizi na kufanya mahojiano na Mganga mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo Dr. Msafiri Kimaro, ambaye alisema kuwa hakuwa na taarifa.

Baada ya mahojiano zaidi Dr. Kimaro alimchukua mwandishi na kuongozana naye kwenda wodini kwa ajili ya kuangalia nyaraka ambapo alijiridhisha kuwa mjamzito huyo alijifungua salama na mtoto alikuwa salama lakini pia katika jarada la Paulina wataalam hao wameandika kuwa hawajaona sababu yeyote iliyosababisha kifo cha mtoto huyo.

“Ninakuomba siku ya Alhamisi (Machi 31, mwaka huu), ufike kwa ajili ya taarifa zaidi ili nifuatilie” alisema Dr. Kimaro.

Machi 31, mwaka huu, tayari timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya ilifika katika hospitali hiyo kuhoji jambo hilo na mengine ambayo gazeti hili linaendelea kujiridhisha likiwemo mwanamke aliyefanyiwa upasuaji na kushindwa kushonwa vizuri na sasa tumbo lake limeanza kuvimba na anatakiwa kufanyiwa upasuaji mpya ili ashone vyema katika hospitali ya wazazi Meta.

April mosi mwaka huu, mwandishi alifika tena hospitalini hapo na kukutana na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dr. Msafiri Kimaro na Katibu wa Hospitali hiyo, Dick Balagasi, ambapo walisema maelezo yote mwandishi anapaswa kuyapata kwa wauguzi waliokuwa zamu maana wao hawakuwepo siku tukio hilo likifanyika.

“Kalulunga lakini unapaswa kudumisha mahusiano na nasi maana tumeambiwa kuwa unaishi jirani hapa, hivyo ni vema tukadumisha mahusiano kuliko ukisikia jambo unaandika” alisema Balagasi kabla hajakatishwa na kauli ya mwandishi wa habari kuwa “Hisia zisiondoe uhalisia”.

Hata hivyo ikumbukwe kuwa, mtindo wa uongozi wa Hospitali hiyo kuwa na kifua kikubwa cha kuwatetea baadhi ya watumishi wanaoshindwa kuwajibika vizuri ulisababisha mjamzito Sabina Mwakyusa (28), kufukuzwa wodini na kujifungulia katika geti la hospitali hiyo kwa msaada wa walinzi huku mvua ikinyesha usiku.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Desemba 19, mwaka 2013, ambapo baadhi ya wauguzi waliokuwepo katika chumba cha matazamio ya kujifungua, walidaiwa kumfukuza na kumpiga mjamzito Sabina Mwakyusa(28) mkazi wa Kijiji cha Iwala, kata ya Utengule Usongwe wilayani humo.

Sabina, alisema alifika hospitalini hapo Desemba 18, 2013 na alipimwa na manesi ambapo walimwambia kuwa hawamuoni mtoto tumboni mwake.
‘’Baadaye akaja Daktari na kunipima, akaniambia mtoto anaonekana vizuri na ningejifungua mtoto wa kike ndipo nikaendelea kusubiri uchungu zaidi’’ alisema Sabina.

Alisema ulipofika usiku wa Desemba 19 majira ya saa mbili usiku, alianza kujisikia uchungu, ndipo manesi waliompima mwanzo wakamwambia anatakiwa apimwe tena jambo ambalo alikataa kwa madai kuwa alikuwa akiumizwa, ndipo wakamwambia aondoke hospitalini hapo kwasababu ana kiburi.

‘’Baada ya kuonekana mimi nasita kuondoka, wakaanza kunipiga na kunipatia biki na kunilazimisha kuandika kuwa mimi sitaki kujifungulia hapo ndipo tukatoka na mama na kwenda nje ya geti na kujifungulia getini huku mvua ikinyesha’’alisema Sabina Mwakyusa.

Alisema, mama yake na baadhi ya wajawazito waliokuwepo ndani ya wodi hilo, walijaribu kuwabembeleza wasimfukuze lakini walikataa. 

Mama mzazi wa mwanamke huyo, Roda Mwakyusa(50), alisema anaumia akikumbuka yaliyomkuta mwanaye ikiwa ni uzao wake wa kwanza.

‘’Niligaragara mweeeh! kuwaomba msamaha wale manesi ili wamsamehe na kumhurumia huyu mtoto wangu, lakini walikataa wakisema kuwa ana kiburi sana’’ alisema Prisca Mwakyusa.

Alisema walipotoka wodini huku mwanaye uchungu ukimzidi, walifika getini akazidiwa. Chupa ikapasuka. Damu zikaanza kumvuja; alikaa muda mrefu zaidi ya saa moja na kuanza kujifungua ndipo walinzi wa kampuni ya Mult-Lion, wakamsaidia kumpeleka katika upenu wa duka la hospitali hiyo ili kukwepa kokoto zilizopo na mvua iliyokuwa ikinyesha.

Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Mult-Lion, Kinanda Sanga, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema kuwa hakuwa na taarifa lakini baada ya kuwauliza askari wake walimpatia taarifa ya tukio hilo kuwa lilitokea na wao wakatoa msaada.

Dada wa msichana huyo, Enitha Mwakyusa(35), alisema alipigiwa simu majira ya saa tano usiku na mama yake mzazi akimweleza yaliyomkuta mdogo wake na kwamba atafute gari la kwenda kuwachukua.

‘’Mama alinipigia simu usiku, nikawaamusha majirani ambao walikuwa na namba za madereva tax, ambapo saa saba walifika hapa nyumbani Mapelele’’ alisema Enitha.

Wifi wa Sabina Mwakyusa, Prisca Nafred, alisema alimpeleka mtoto aliyezaliwa katika hospitali hiyo majira ya saa saba mchana ya Desemba 20, kwa ajili ya chanjo, lakini hakupata chanjo kwa madai kuwa alikuwa amechelewa kufika, hivyo alitakiwa kufika siku ya Jumanne Desemba 24, mwaka huo.

Desemba 21, familia hiyo ilimpigia simu Mwandishi wa habari wakimweleza kuhusu maendeleo mabaya ya mtoto ambapo Mwandishi wa habari hizi alimtaarifu Mratibu wa afya ya mama na mtoto mkoa wa Mbeya, Prisca Butuyuyu, kuhusu suala hilo ambapo makubaliano yaliafikiwa kuwa mtoto apelekwe Hospitali ya Rufaa, kitengo cha wazazi Meta.

Mtoto huyo alipokelewa Meta na kuingizwa kwenye chumba cha joto kisha kuanza kupatiwa matibabu kwa kuwekewa drip za maji mpaka Desemba 23 mwaka huu.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbeya Louis Chomboko, alipopata taarifa, alichukua hatua ya kwenda kumuona mtoto huyo katika hospitali ya Meta.
‘’Nimeonana na mama wa mtoto na kumuona mtoto chumba cha joto na kupata maelezo yote ikiwa ni pamoja na maelezo ya file la Meta hivyo nipe nafasi tena kufuatilia tukio hili hospitali ya Ifisi na tukibaini ukweli tutachukua hatua’’ alisema Dr, Chomboko akimsihi Mwandishi kutoandika kwanza habari hii.

Mwezi Desemba mwaka 2012, Mama mmoja(jina tunalo), aliyekuwa anaumwa BP, alichomwa sindano (dawa)ambazo haziendani na ugonjwa wake na mmoja wa watoto wake alipohoji kwa uongozi wa hospitali hiyo alijibiwa kuwa hapaswi kugombana na wauguzi! Kisha akaitwa Dr. Kenneth, ambaye aliamua kuokoa maisha ya mama huyo katika hospitali hiyo ya Ifisi kwa kumchoma sindano ya dawa iliyokuwa ikitakiwa.

No comments:

Post a Comment