Tuesday 5 July 2016

TACOMO KWA KUSHIRIKIANA NA WOMEN FUND TANZANIA WATOA MAFUNZO YA UONGOZI NA HAKI KWA WANAWAKE NA WASICHANA WANAOFANYA BIASHARA KATIKA MASOKO MPANDA MKOANI KATAVI

SERA ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 ni moja wapo ya miongozo ya serikali katika jitihada za kuwapa wananchi mwelekeo wa Maendeleo ya wanawake na jinsia utakaohakikisha kuwa sera, Mipango, Mikakati na shughuli mbalimbali za maendeleo katika kila sekta na taasisi katika  ngazi zote zinazingatia usawa wa jinsia.

Sera hiyo inachukuwa nafasi ya sera ya Wanawake katika maendeleo ya mwaka 1992 ili kuingiza dhana ya jinsia katika maendeleo ya jamii.

Dhana  ya jinsia ni mtazamo mpya wa kuharakisha maendeleo kwa
kuangalia mahusiano ya jamii kati ya wanawake na wanaume ambayo yanatambua tofauti zilizopo za kijinsi (sex) baina yao pamoja na mgawanyo wa majukumu katika jamii.

Ili kuweza kupata maendeleo ya haraka na endelevu dhana ya jinsia pia inatilia mkazo umuhimu wa kushirikiana na kufanya kazi kwa kutegemeana kati ya wanawake na wanaume.

Hii inatokana na ukweli kuwa, majukumu ya wanawake katika jamiini tofauti nay ale ya wanaume na kuwa yote ni muhimu kwa maendeleo ya familia, jamii na Taifa.

Mwelekeo wa maendeleo ki-jamii, kitaifa na ki-mataifa hivi sasa
unasisitiza na kuhimiza upangaji na utekelezwaji mipango unaozingatia ushirikishwaji wa wanawake na wanaume kwa pamoja katika kutambua, kuthamini na kukuza vizuri zaidi uwezo wa wananchi katika kujiletea maendeleoyao.

Utekelezaji wa sera hiyo unazingatia mchango wa sekta mbalimbaliu za serikali na zisizo za serikali, wataalam mbalimbali wakiwemo wasomi na wanataaluma na watu binafsi wanawake na wanaume. Msukumo upo kwenye kuingiza masuala ya jinsia (Gender Mainstreaming) na kuhakikisha kuwepo kwa shughuli mbalimbali zinazowalenga wanawake (Woman Specific)
ili kuharakisha kuwepo usawa wa kijinsia unaotarajia.

Kutokana na sera hiyo kuelezea pia kuhusu mashirika yasiyo ya
kiserikali kuhusika katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya
wanawake na jinsia, shirila lisilo la kiserikali la Tanzania Community Media Organization(TACOMO), limetoa mafunzo ya kukuza sauti na kuwaimarisha haki za wanawake na wasichana kushiriki nafasi za uongozi katika maeneo ya Masoko ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, chini ya ufadhili wa Woman Fund Tanzania.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yalifanyika katika ukumbi wa Shule ya
Sekondari ya St. Mary’s ya Kashaulili huku wanawake 80 na wanaume 11wakishiriki katika mafunzo hayo na mdahalo.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Gordon Kalulunga ambaye pia ni Mwandishi wa habari aliyebobea katika nyanja za habari za Afya ya uzazi na dawa za kulevya nchini, aliwataka wanawake na wasichana waliokuwa wameshiriki katika mafunzo hayo, kuwa majasiri na kushiriki katika kuwania nafasi za uongozi ili kuweza kupaza sauti zao.

“Shime natoa kwenu, jitokezeni katika kuwania nafasi za uongozi katika nyanja zote kuanzia huko sokoni, mahala mnapoishi na wale ambao wana vyama vya siasa pia jitokezeni na anapojitokeza mwanamke wanawake wengine muungeni mkono kwa kumchagua”alisema Kalulunga.

Aidha alisema kuwa kuna changamoto kubwa ambao anaiona kwa wanawake wengi kuwa ni uwoga ambao unatokana na viongozi wa serikali hasa ngazi za mitaa, Vijiji na wilaya kutowajulisha wananchi majukumu yao kama viongozi hivyo wananchi hasa wanawake wanabaki katika kifungo cha woga hata wa kuhoji wakihofia misukosuko ya viongozi wa serikali wasio waadilifu.

Wakati anayasema hayo, Ofisa Maendeleo ya jamii wa kata ya Kashaulili na majengo ambaye pia alikuwa mwezeshaji, Imelda Mkama, alipotakiwa kuwaeleza washiriki wa mafunzo hayo majukumu yake ili wafahamu na kuhamasika kuoimba ushauri kutokana na kazi zake, alikataa katu katu na kwamba atakutana nao siku nyingine.

Akitoa mada ya ujasiliamali na uongozi, Ofisa huyo aliwataka wanawake hao kuwa hodari katika kuthubutu.

“Wajasiliamali wengi si wabunifu bali wanaiga biashara. Tusiwe na
biashara moja maana ukimwezesha mwanamke mmoja, umewezesha watu 10.”Alisema Imelda.

Aidha alitoa elimu ya uundwaji wa vikundi kwa wanawake hao na
kuwaambia kuwa pesa ambazo zinatarajiwa kwenda kila kijiji maarufu kama Milioni 50 za Magufuli, hazitagawiwa kwa mtu mmoja mmoja bali zitakopeshwa kwenye vikundi ambavyo vimesajiliwa, hivyo kwa wale ambao wanahitaji kusajili vikundi na kuandika katiba, milango ipo wazi katika ofisi yake.

Katika masoko ya Buzogwe na Mapnda Hoteli, uchaguzi wa uongozi wa masoko hayo unatarajiwa kufanyika June 30, mwaka huu ambapo wanawake kadhaa wamehamasika kuwania nafasi mbalimbali huku wakisema kuwa wanahitaji zaidi elimu na mafunzo kama yaliyotolewa na shirika la TACOMO.

Mwenyekiti wa Soko la Mpandfa Hotel, Boniface Mganyas, ambaye ni mkazi wa Majengo, anasema kuwa wanawake wengi huko nyuma walikuwa na woga wa kujitokeza katika kuwania nafasi za uongozi lakini baada ya semina hiyo tayari wanawake wawili wamejitokeza kujaza fomu za uongozi.



 Naye Mwenyekiti wa soko la Buzogwe, Ramadhan Karata, anasema kumekuwa na changamoto kubwa kuwapata viongozi wanawake ambao baadhi wanazuiliwa na waume zao kuwania nafasi za uongozi.

“Mafunzo kama haya yakiendelezwa yatasaidia sana kuwaondoa wanawake uwoga wa kujitokeza kuwania nafasi za uongozi katika jamii maana wengi hawana elimu za kutosha ili hali wana hulka za uongozi, hivyo naomba TACOMO mrudi tena na tena na muende katika maeneo mengine kuwahamasiha wanawake ili waweze kujitokeza na pale kwenye soko letu mwanamke mmoja
amesema nimjazie fomu” alisema Karata.

Mkufunzi wa mada ya haki za wanawake, William Simwali, ambaye anaishi na ualubino, aliwataka wanawake hao kuondoa woga kujitokeza katika uongozi na kwamba wajifunze kwa wanawake wenzao ambao ni viuongozi katika Taifa hili na wote wanaweza.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo Mwasiti Mohammed, alisema yeye kabla ya uchaguzi wa masoko hayo, atajitokeza pamoja na baadhi ya wanawake wenzake kwenda kuishamilisha elimu aliyoipata kutoka TACOMO na kwamba yeye pia mwaka 2017 atawania nafasi ya uongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Wanawake wengi tunahitaji elimu kama hizi, hivyo naona kuna haja ya kuwafuata wanawake huko huko waliko na kutoa elimu hizi za uongozi za kukuza sauti na kuwaimarisha haki za wanawake na wasichana kushiriki nafasi za uongozi katika maeneo ya Masoko ya Manispaa ya Mpanda”alisema Mwasiti.

No comments:

Post a Comment