Lusiana Danda
(26) alipokuwa na Ujauzito wa miezi nane (Oktoba 2012), alikuwa anatokwa na damu
ya mwezi.
Hali hii ambayo
ni hatarishi kwa mjamzito na mimba yake ilianza ujauzito ukiwa na miezi
minne, baada ya kuugua malaria.
Lusiana, ambaye ni mkulima na mkazi wa
kijiji cha Ifinga, Songea mkoani Ruvuma, alipata matibabu katika zahanati ya Ifinga.
Alivyokutwa na
malaria, alipewa dozi ya dawa ya mseto ambayo hakuimaliza. “Niliamua kuacha
kumeza dawa baada ya kusikia naendelea vema. Pia, nilipokuwa
nameza dawa hizo nilikuwa nasikia maumivu chini ya kitovu; nikahofia mimba
yangu isije kutoka,” alisema Lusiana.
Dada huyu hakuwa na mume na hakuwa na mahusiano na mwanaume aliyempa mimba aliyokuwa nayo wakati huu.
Kwa
kuwa tayari alikuwa na watoto wawili na pasipokuwa na mtu mwingine wa kumtegemea,
Lusiana aliendelea na kazi za kulima kama kibarua bila ya kupumzika, japokuwa
alikuwa mjamzito na anaumwa.
Anasema siku moja,
Lusiana akiwa shambani na baada ya kulima kwa saa mbili, ghafla aliaanza
kusikia maumivu makali chini ya kitovu.
Maumivu hayo
yalikuwa yakizidi kadiri muda ulivyokwenda na alikuwa akijisikia hali ya kutaka
kujisaidia haja ndogo.
Alipoenda msalani
kujisaidia, ndipo akashtukia kuwa haukuwa mkojo bali ilikuwa ni damu. Damu hii
iliendelea kutoka kidogokidogo kwa siku tatu bila kukatika, ndipo Lusiana
aliamua kwenda zahanati ya Ifinga kupima kama ujauzito wake bado ulikuwa
salama.
“Nilipofika
zahanati niliambiwa nitoe Tsh. 2,000 ili nipimwe kujua kama mimba bado ipo.
Nilikuwa sina pesa kwa hiyo nilirudi nyumbani nikiwa sina raha,” alisema
Lusiana.
Japokuwa damu
ilikoma kutoka siku hiyo hiyo ya tatu, baada ya wiki mbili, Lusiana alifanikiwa
kupata Sh10, 000 na kurudi tena kwenye zahanati kufanya kipimo cha ujauzito.
Kipimo kilionesha
kwamba bado alikuwa mjamzito lakini, mwezi uliofuata damu iliendelea kutoka
tena na Lusiana aliporudi kwenye zahanati ya Ifinga kwaajili ya kujua kwa nini,
hakufanikiwa.
“Niliambiwa
hakuna vifaa vya kuchunguza kujua kama damu inayotoka inasababishwa na nini; na
mhudumu wa afya aliniambia kuwa hajasomea kujua damu inayotoka kwa mjamzito
inasababishwa na nini,” alisema Lusiana.
Kwa mujibu wa Dk.
Ahmed Makuani, mtaalam wa magonjwa ya wanawake na uzazi salama kutoka Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, kutokwa na damu kwa mjamzito ni kiashirio cha hatari
sana.
Mjamzito akiona
damu inatoka anatakiwa kuwahi haraka hospitali. Dk. Makuani alisema wanawake
walio na umri wa zaidi ya miaka 35 wakishika mimba wako katika hatari ya
kupoteza damu kwa sababu ya kondo la nyuma kuning’inia katika shingo ya kizazi
upande wa ndani.
Tatizo hili
linajulikana kama placenta previa. Kitendo cha kondo la nyuma kuvumba kinaweza
kusababisha kuachia sehemu iliyojishika na kutoa damu sehemu ile iliyoachia,
pamoja na kuziba njia ya uzazi kuwa ndogo na mtoto kushindwa kutoka vizuri, kuzaliwa
mtoto mfuu kwa kukandamizwa na kondo hilo, kuzaliwa mtoto njiti pamoja na
kuzaliwa mtoto mwenye uzito mdogo.
Naye aliyekuwa Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid anasema kuwa tatizo la
mjamzito kupoteza damu ni tatizo sugu na kubwa sana hapa nchini Tanzania na
ndio chanzo kikubwa cha wajawazito kufariki.
Dk. Rashid
alisema kuwa, wataalam wa kulitatua tatizo hilo wapo wachache sana katika
zahanati mbalimbali za vijijini ambako asilimia 75 ya watanzania ndio wanaishi
huko.
“Kwa sasa tupo
katika mkakati wa kuboresha zahanati mbalimbali kwa kuwapeleka watumishi wa
sekta ya afya kusoma, masuala ya uuguzi kwa miaka miwili ili muuguzi
anapokutana na tatizo hilo awe na ujuzi wa kumsaidia mjamzito,”alisema Dk.
Rashid.
Wakati Sera ya
Afya ya 2007 inasistiza utoaji wa huduma bora na bure kwa mjamzito, hili bado
ni changamoto kwa maeneo kama Ifinga, Songea.
Zahanati ya
Ifinga ina nesi mmoja na muhudumu wa afya aliyefika darasa la saba mmoja. Pia,
katika zahanati hiyo, kuna mganga moja na mpimaji magonjwa maabara mmoja.
Hakuna mtaalam wa
magonjwa ya mjamzito na wala hakuna vifaa tiba kama mashine ya kumsaidia mtoto
kupumua akizaliwa.
Kwa wakati huu,
ambapo Lusiana alikuwa ni mjamzito na kuhitaji huduma hizi, kulikuwa hakuna
dawa za kumchoma sindano mama ili mfuko wa uzazi usinyae baada ya kujifungua na
mzani wa kupimia mtoto akizaliwa mbovu.
Japokuwa
ameshindwa kupata ufumbuzi wa tatizo lake, Lusiana anatarajia kujifungua katika
zahanati ya Ifinga. Hana uwezo wa kwenda katika hospitali ya Peramiho
inayomilikiwa na Kanisa Katoriki Jimbo la Ruvuma, ambapo ni kilometa 243 kutoka
katika kijiji cha ifinga.
Nauli ya kwenda
ni Tsh.38,000 na gharama za kujifungua ni Tsh. 11,000; hapo bado gharama za
kuishi. Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songea Dk. Daniel Masawe alisema kuwa
katika wilaya hiyo, wajawazito 95 kati ya 100,000 kila mwaka wanapoteza maisha
kwa sababu ya upungufu wa damu.
Alithibitisha
kwamba vifo hivi vinachangiwa na ukosefu wa vifaa tiba pamoja na wataalam wa
kumsaidia mjamzito kujifungua salama katika zahanati mbalimbali kwenye wilaya
hiyo. "Kwa sasa watalaam wa kumsaidia mjamzito kujifungua salama ambao
wamebobea katika ukunga hapa Songea ni wanne tu, ukilinganisha na zahanati 35
tulizonazo," alisema Dk. Masawe.
Mtaalam wa magonjwa ya akinamama katika hospitali
ya Peramiho Dk. Marieta Mtumbuka alisema kuwa mwezi Septemba mwaka 2012,
wajawazito wawili walifika katika hospitali hiyo wakiwa na tatizo la kupoteza
damu.
Kati ya hao ni
mmoja alikuwa na miaka 37. Mjamzito akiumwa malaria na kucheleweshwa au kutokumaliza
matibabu, anakuwa hatarini kupatwa na tatizo la kutokwa na damu.
Ndiyo maana, kwa
mujibu wa Dk. Rashid kuna umuhimu wa mjamzito kutumia dawa ya mseto kwa sababu
ndio dawa pekee iliyofanyiwa utafiti na kugundulika inaweza kutibu na kumkinga
mjamzito na mtoto aliye tumboni na malaria akitumia kipindi ambacho haumwi
malaria.
“Wizara imeamua
kupitisha dawa ya mseto baada ya tafiti mbalimbali kubaini dawa ya chloroquin
inausugu wa kuzoeleka na wadudu wa malaria. Tulipotoka katika dawa ya
chloroquin tukaanza matumizi ya dawa ya fansider lakini nayo ikaonesha uwezo
mdogo wa kukabiliana na wadudu wa malaria.
Baada ya utafiti
ndio tumegundua dawa mbadala ya kumkinga mjamzito na malaria ni dawa mseto,”
alisema na kuongeza kuwa mjamzito anapewa dawa ya mseto akiwa na mimba ya wiki
20 na wiki ya 28.
Katika kitabu cha
hotuba ya makadilio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2012/2013,
kinafafanua kuwa jumla ya dozi 9,196,080 za dawa mseto pamoja na kusambaza
vyandarua vya hati punguzo vyenye viuatilifu 5,412579 kwa wanawake wajawazito
lakini Lusiana hana chandarua.
"Nilipoanza
kwenda zahanati kupima ujauzito wangu, sikupewa chandarua. Niliambiwa
vimekwisha na sina uwezo wa kununua chandarua hivyo nalala bila ya kutumia
hicho chandarua,"alisema Lusiana.
Aidha kwa mujibu
wa bajeti ya afya ya mwaka 2012/2013, kumekuwa na ongezeko la vituo vya afya na
zahanati za serikali na binafsi, kuanzia mwaka 2005 kutoka zahanati 4,322 hadi
zahanati zahanati 4,679 mwaka 2012.
wa upande wa
vituo vya afya, kumekuwa na ongezeko kutoka 481 mwaka 2006 hadi kufikia 742
mwaka 2012 na kwa upande wa hospitali kutoka 219 hadi kufikia 241.
Source; Gordon Kalulunga