Saturday 14 November 2015

Tacomo inawalinda watoto kwa njia ya kuwakusanya kwenye michezo pia

large.jpg Watoto kama hawa wanastahili kuendelezwa vipaji vyao kama wanavyoonekana, hawana viatu lakini duh! mambo safi.

Tusiuze wala kujenga katika maeneo ya wazi ambayo watoto wanacheza.

Dawa za kulevya zaleta uchugu kwa vichanga na wajawazito Tanzania



NA GORDON KALULUNGA.

DAWA za kulevya ni kemikali za majimaji, majani au unga wenye kemikali zenye vilevya, ambazo zikitumiwa na viumbe, hubadili hisia, fikra na tabia ya mtumiaji, akiwemo binadamu na viumbe vingine.

Zinaweza zikawa halali au si halali, asili au zinazotengenezwa kiwandani, katika mfumo wa vidonge, unga au maji, zikatumika kwa njia ya kujidunga, kunusa, kula, kunywa, kuvuta, au kupiga bamba.

Dawa hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo yanatenganishwa kutokana na jinsi dawa hizo zinavyoathiri mfumo wa utendaji kisaikolojia (psychoactive substance).

Makundi hayo ni Vichangamshi (Stimulants) mfano; cocaine, tumbaku na khat.


Kundi la pili ni Vipumbaza (Depressants), mfano; pombe, heroine, methadone, codeine, morphine, na gundi.

Kundi la tatu ni Vileta Njozi (Hallucinogens). Mfano ; uyoga, bangi.

Wanawake wajidunga waeleza yaliyowapata wakati wa ujauzito.
Baadhi ya wanawake wanaotumia dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam, na walioacha kutumia, wanaeleza adha na changamoto wanazozipata katika maisha yao ndani ya jamii.

Wanasema, walijitumbukiza katika matumizi ya dawa hizo bila kujua kuwa ni utumwa na ugonjwa mbaya.

Fatuma Athuman, mama wa mtoto mmoja wa kike, anasema alianza kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin kwa kuchanganya na sigara huku akivuta, kisha akaanza kujidunga na sindano na hatimaye Baba yake akamfukuza nyumbani, akaenda mitaani ambako pia alikuwa akiambulia mateso ya polisi ya kukamatwa na kupigwa.

“Mwaka 2012 ndipo nilipotamani kuacha kutumia dawa za kulevya, nikajipeleka kwenye tiba ya Methadone inayopatikana Mwananyamala, Temeke na Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, kwa sasa naendelea vizuri”anasema Fatuma Athuman.


Fatuma Side(31), anasema alianza kutumia bangi akiwa na miaka 25, na hakuwa na mtoto, baadaye akaaza kutumia Cocain na sasa ana mtoto.

“Nilipata mimba nikiwa nyumbani, lakini kipindi hicho nilikuwa nashinda sana maskani kuvuta. Nilipojifungua nikaendelea kwenda na mtoto huko maskani, lakini ikanishangaza mtoto alipoanza kupata akili, akawa anaiga vitendo vyote tulivyokuwa tukifanya maskani…, nikaanza kumwacha nyumbani kwa wazazi wangu ili asiharibike”anasema Fatuma Side.

Anasema katika maisha yake ya utumizi wa dawa za kulevya, anakumbuka kuwa aliuza vitu vyake vya ndani ili ajipatie pesa kwa ajili ya  kununua dawa za kulevya!

Wajawazito na ulalaji katika maskani za kuvutia dawa za kulevya
Fatuma anasema, ulalaji wa wanawake wenye mimba na watoto huko  maskani siyo mzuri, mwanamke mmoja analala katikati ya wanaume kumi, huku mtoto akiwa anapigwa na baridi kwa sababu siku nyingine usiku kunakuwa na baridi kali, huku wengine wakiendelea kuvuta bangi na wengine wakijidunga.

“Ukiwa na mtoto mdogo maskani ni shida sana, unalala mwanamke peke yako katikati ya wanaume kumi huku mtoto mchanga akipigwa na baridi, unaamka asubuhi mama mtu miguu ikiwa imevimba na wakati huo huo utakuta umelala saa nane usiku baada ya kutoka labda stereo au Muhimbili kutafuta unga” anasema Fatuma Side.


Anaeleza kuwa amewahi kukamatwa na askari polisi na kupelekwa gereza la segerea kwa siku ishirini, ambako anasema maisha ya huko hayana utu kabisa, kisha siku ya ishirini alipopelekwa mahakamani akaachiwa huru.

Anasema, mtumiaji wa dawa za kulevya ana hatari ya kupata maambukizi ya VVU na homa ya ini B na C, kutokana na ngono na udungaji usio salama ambao unasababishwa na matumizi ya kuchangia sindano za kujidungia na kwamba uzoefu wake mpaka sasa wengi wa wajidunga wana maambukizi ya VVU na kifua kikuu kutokana na tabia za kulundikana kulala na kufanya ngono zisizo salama na baadhi ya wanawake kufanya biashara ya ngono isiyo salama.

Kwa sasa anasema ameacha kutumia dawa za kulevya, kutokana na msaada na huduma anazozipata kutoka shirika la Medecins du Monde (MDM), na anaishi kwenye nyumba yake aliyojenga, bado hajaolewa, wadogo zake na wazazi wakimuona hawalii tena, jamii inamuheshimu si kama zamani.

Kwa sasa nimwelimishaji rika wa MdM na ana wahudumia wenzake kwa kuwapa elimu ya afya, kondomu na vifaa salama vya kujidungia hasa ambao wanaendelea kutumia dawa za kulevya na anasema wengi wanabadilika ikiwemo kupunguza matumizi na kuacha kabisa kama yeye.

Mbali na huyo, Salima Hamad (30), anasema yeye amevuta bangi kwa kuchanganya na heroin kwa miaka 14, na amejidunga kwa muda wa miaka 5.

Anasema “nilipo anza kutumia dawa za kulevya, mwanzoni hakuna aliyegundua, siku zilivyokwenda nilianza kudhoofika kiafya, mama aliambiwa kuwa mwanao anatumia dawa za kulevya, aliponiuliza, nikamkatalia lakini siku zilivyokwenda afya yangu ilianza kudhoofika, nyumbani walithibitisha kuwa natumia dawa za kulevya walikuwa wakinisema sana, nikaondoka nyumbani,”anasema Salima.

Anasema katika maisha ya utumiaji wake, alinyanyapaliwa, kila alipokuwa akipita hasa maeneo ambayo wanamfahamu alikuwa anasemwa vibaya kwa dharau kuwa siku hizi ni mwizi, mtu yeyote asimuamini.

“Niliumia sana, kwani hakuna mtu aliyekuwa akiniamini, kwani jamii ishakuwa na mtazamo kuwa kila mtumiaji wa dawa za kulevya ni mwizi”.anasema.

Yeye akiwa mwanamke mtumiaji wa dawa za kulevya, alipokuwa mjamzito kwa mara ya kwanza hakuwahi kwenda kliniki kwa sababu ya hofu ya kuwaeleza wahudumu jinsi gani wangeweza kumwelewa wakati hakuwa na fedha.

“Kwa muonekano wangu, nilijipa majibu kuwa nesi hawezi kunijali, kwahiyo niliendelea na maisha ya maskani mpaka nikajifungulia huko huko, sikuwa na chakula cha mtoto, hivyo hivyo nikipata haya, nikikosa sawa, huku nilikuwa nikiendelea kutumia dawa za kulevya” anasema Salima.
Alipoulizwa kuwa nani alimsaidia wakati wa kujifungua, anasema ni wenzake. 

Dr. Moke Magoma wa shirika la Evidence For Action(E4A) linaloshughulika na mradi wa kuokoa maisha ya mama na mtoto nchini(Mama Ye!), ambaye ni mbobevu wa masuala ya afya ya uzazi, anasema robo tatu ya wajawazito wanaobeba mimba na kujifungua, wanajifungua salama bila hata wasaidizi wenye ujuzi bali robo inayobaki ndiyo wanapata shida na baadhi kufariki.

“Bahati mbaya ni vigumu kuwatambua wale robo kwasababu matatizo hutokea ghafla na bila kutegemewa hivyo haja ya akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya afya vyenye wataalam wenye ujuzi wa ukunga ni muhimu ingawa bahati mbaya bado kuna vituo hasa vijijini havina wataalam maana siyo kila mhudumu ni mkunga” anasema Dr. Moke Magoma.

Katika ujauzito wake wa pili, Salima anaeleza kuwa akafahamu kuwa kuna shirika la MdM linalosaidia wajidunga, alikwenda huko na akahudumiwa kama mtoto, akapelekwa hospital, akapatiwa vifaa vya kujifungulia na akawa anafuatiliwa mpaka akajifungua huku akipatiwa pia unga wa uji na chakula cha kwake na mtoto.

Kwa sasa anasema anatumia dawa aina ya methadone, inayosaidia kupunguza kiasi cha matumizi ya dawa za kulevya na kuacha, anasema amebadilika hata mwili wake, anaenda kwenye kituo cha MdM kupatiwa elimu na kupimwa kuangalia hali yake ya maambukizi.

“Kwa ufupi kutokana na mradi huu tunaonekana sasa watu, hata nikienda nyumbani wanaongea na mimi kama mtu mwingine”anasema. 

Mtaalam wa mifumo ya kompyuta katika Tume ya uratibu na udhibiti dawa za kulevya Tanzania bara, January Ntisi, (DCC), anasema matumizi ya dawa za kulevya nchini yanasababishwa na sababu tofauti ikiwemo makundi rika, unyanyasaji wa kisaikolojia wanaofanyiwa watu, upungufu wa maadili mema, ushawishi, kuonesha ufahari na mambo mengi.

Anasema, urefu wa ukanda wa bahari wenye vipenyo vingi ni moja ya sababu ya dawa hizo kuendelea kuingia nchini.

Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa, mazingira ya bandari ya Zanzibar ni tatizo katika kufanikisha kupunguza uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya kutokana na bandari hiyo kuwa wazi kiasi ambacho mtu yeyote anaweza kuingiza kitu chochote nchini mbali na dawa za kulevya.

Ofisi ya kamanda wa polisi Mkoa wa Unguja Zanzibar, inakiri kuwa, uingizaji wa boti zaidi ya moja kwa wakati mmoja bandarini ni moja ya kikwazo katika kupambana na wahalifu na kwamba mazingira ya Kijiografia ya visiwa vya Zanzibar yanachangia kwasababu kuna zaidi ya bandari 500 za kienyeji Unguja pekee, ambazo zinaweza kuingiza madawa ya kulevya kwa kutumia vyombo vidogo vidogo vya kienyeji wakati wowote ule wapendao, na kwa sababu Polisi haina vyombo vyovyote vya kufanyia doria ni vigumu kufika maeneo kama hayo ambayo kwa hakika yanatakiwa uangalizi wa mara kwa mara. 

Watumishi wa MDM waeleza huduma waitoayo
Mfanyakazi (Outreach Worker) wa shirika la Medecins du Monde(MdM) la wilayani Temeke, Aina Mrope, anasema anaumia kuwaona wanawake wanaotumia dawa za kulevya huku wakiwa na familia.

“Tunawaendea hata majumbani na kuwasaidia kuwapa elimu ya afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka hospitali wale wanaoumwa na kuwapatia kondomu wale ambao wanafanya biashara ya ngono”anasema Aina.

Anasema wanawake wanaotumia dawa hizo za kulevya na kuhudumiwa na kituo chao, wanapatiwa pia pamba, nguo, chakula, dawa za nywele, mafuta, vipodozi na kila siku kuu wanapatiwa mavazi.

Mshauri wa masuala ya saikolojia wa shirika hilo la MDM, Benjamin Myovela, anasema moja ya kazi zinazofanywa na kitengo chake ni kuwashauri watumiaji madhara ya udungaji usio salama na hatari zake, ambapo jambo la kuamua kuacha au kuendelea ni la muhusika mwenyewe, lakini akiwa bado anatumia atumie kwa njia ya usalama ili asipate maambukizi ya VVU na homa ya ini B na C au matatizo mengine ya kiafya. 
Mshauri wa masuala ya afya wa shirika hilo, Prof. Joseph Mbatia, anasema kuwa kundi la wanaotumia dawa za kulevya lipo katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU.

Anasema kundi hilo likiachwa bila kupewa elimu na kusaidiwa katika matibabu na kujikinga, jamii itakuwa kwenye hatari zaidi kwasababu kuna baadhi wanafanya biashara ya ngono.


“Kuna wanawake wanaotumia dawa za kulevya na kufanya biashara ya ngono kwa lengo la kupata fedha, wanakutana na watu ambao hawatumii ambao pia endapo mwanamke huyo ana maambukizi, jamii nzima inakuwa hatarini” anasema Prof. Mbatia.

Meneja wa mafunzo wa shirika hilo, Damali Lucas, anasema“matatizo kwa wanawake wanaoutumia dawa za kulevya ni mengi sana, muda mwingi jamii inawalaumu na kuona kuwa maisha wanayoishi wanajitakia au wamependa.


“Kama jamii hatukumbuki kuwa kuna wengine wameingia katika matumizi ya dawa za kulevya kwa ushawishi kutoka kwa wapenzi wao, wamefiwa wazazi wao, kwa hiyo hawakuwa na uangalizi mzuri.” Anasema Damali.

Anasema, wanawake wanaotumia dawa za kulevya wanakumbwa na matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa kupigwa hasa na wapenzi au hata watu kutoka kwenye jamii, wanachukuliwa kama wamama ambao hawawezi kulea watoto, kuna wengine wakijifungua watoto wananyang’anywa kwa madai hawawezi kulea.


“Kwa sasa MdM inajitahidi sana kuwafikia wanawake wanaotumia dawa za kulevya popote walipo majumbani kwao na kituoni kwa sababu kutokana na utafiti uliofanyika kiwango cha maambukizi ya VVU kwa wanawake wanaotumia dawa za kulevya kipo zaidi ya asilimia 60%, kwa hiyo ni hatari sana kwa afya ya jamii kwasababu wanaingiliana na watu wa kawaida hata kwenye masuala ya kingono” anasema Damali.


Pia anasema MdM inatoa huduma za kisheria kwa wanawake wajidunga na walioacha kutumia dawa za kuelvya, huduma za afya ya uzazi, tiba na ushauri wa kisaikolojia ili wawe na afya bora na kuheshimika kama wanawake wengine.

Taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini ya mwaka 2011, iliyotolewa na tume ya kuratibu udhibiti wa dawa za kulevya, chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya kuzuia biashara haramu ya dawa za Kulevya [Sura ya 95], inaonesha kuwa, dawa za kulevya zinazotumiwa kwa wingi nchini ni bangi ikifuatiwa na mirungi, heroin na cocaine.

Dawa nyingine ni kama vile gundi na petrolpamoja na dawa za tiba zenye madhara ya kulevya zikiwemo valium, morphine na napethidine.

Inasema kuwa, matumizi ya dawa hizi yamejikita zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa na Morogoro ambapo wengi wa watumiaji ni vijana wa kiume wenye umri kati ya miaka 12-35.

Taarifa hiyo inasema kuwa, matumizi haya hufanyika kwa siri katika maeneo mbalimbali yakiwemo makaburini, mageto, majengo yasiyokamilika, magofu, vijiweni na viwanja vya michezo.


Makala hii imeandikwa kwa msaada wa mfuko wa vyombo vya habari Tanzania(TMF), Tume ya kuratibu udhibiti wa Dawa za kulevya nchini(DCC) na Dawati la Umoja wa Mataifa la kupambana na mihadarati na uhalifu (UNODC).

Mwandishi wa makala 0754 440749
Email; kalulunga2006@gmail.com

NANI MWENYE HAKI YA KUMBEBA MTOTO KATI YA HAWA WALIOWABEBA WATOTO?


large.jpg

large.jpg

WAZEE HAWA WANATAKIWA KUTHAMNIWA SI KUTUMIKA KATIKA SIASA AFRIKA.

large.jpg

UAKATILI WA KIJINSIA KATIKA PICHA

large.jpg
Je ulevi ndiyo unasababisha haya au umasikini?

FISTULA YATESA WANAWAKE MBEYA.

Mkurugenzi wa Shirika hilo Gordon Kalulunga (kushoto).

Mbeya Vijijini na Mbozi vinara ugonjwa wa Fistula.

  • Serikali itoe elimu na kuwatibu wagonjwa.
  • Mwanamke mmoja ang’olewa kizazi.

ASASI isiyokuwa ya Kiserikali ya Tanzania Community Media Organization (TACOMO) yenye makao makuu mkoani Mbeya, imesema ugonjwa wa matundu sehemu za siri kwa wanawake (Fistula) umekuwa mkubwa mkoani humo hivyo Serikali inatakiwa kuvalia njuga ugonjwa huo unaotibika.

Wakizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya, viongozi wa asasi hiyo wamesema asasi yao imefanya uchunguzi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na kubaini maeneo yenye wagonjwa wengi wa Fistula ikiwemo wilaya ya Mbeya Vijijini na Mbozi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Gordon Kalulunga alisema katika wilaya hizo baadhi ya maeneo ndiyo ulikotopea(komaa) ugonjwa huo na wanawake wengi wanashindwa kujitokeza kutibiwa ugonjwa huo kutokana na elimu duni ya matibabu ya ugonjwa huo ambao matibabu yake yanatolewa bure na Serikali.

Kalulunga alizitaja wilaya za Mbozi na Mbeya Vijijini kuwa ni wilaya za mkoa wa Mbeya zenye wagonjwa wanawake wengi walioathiriwa na ugonjwa huo wa Fistula hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya inapaswa kuchukua hatua za makusudi kuwarejeshea utu wanawake wenye matatizo hayo ya Fistula kwa kuanzisha kampeni yenye tija kwa kushirikiana na Hospitali teule ya Ifisi na Hospitali ya Rufa ya Mbeya kitenmgo cha wazazi Meta.

Aidha alisema mbali na kushirikiana na Hospitali hizo pia Serikali iongeze wataalam katika Hospitali hizo wenye uwezo wa kutibu Fistula tofauti na sasa ambapo Hospitali hizo zina Mganga mmoja mmoja wenye uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

‘’Tumefanya uchunguzi wa muda mrefu tangu mwezi Mei mwaka 2010 na kubaini kuwa wanawake wengi katika wilaya hizo wana Fistula lakini hawajajitokeza kutibiwa kwa kuogopa na wanatengwa katika shughuli za kijamii na baadhi wamekimbiwa na waume zao hivyo tunaiomba Serikali ichukue Jitihada za makusudi kuanzisha kampeni za kuwasaidia wanawake hao zitakazopelekea kupata matibabu na ikiwezekana matangazo yatengenezwe na Haki Elimu’’ alisema Kalulunga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa asasi hiyo Angelica Sullusi alisema ugonjwa huo hutokana na jeraha wanalopata kina mama wakati wa kujifungua baada ya kupata uchungu kwa muda mrefu na pia kuwa na njia ndogo ya uzazi kiasi kwamba kichwa cha mtoto kinashindwa kupita kwa usalama wakati wa kujifungua.

Mgandamizo huo wa mtoto husababisha tundu katika njia ya uzazi na kibofu cha mkojo na mara nyingine katika njia ya haja kubwa na kusababisha muathirika kutoka na haja hizo bila ya mpangilio au kujizuia.

Kutoka huko na haja ovyo, huacha unyevunyevu mwingi katika sehemu za siri na kusababisha harufu mbaya. Wengi wenye tatizo hili hulazimika kuishi kwa hali ya aibu na mara nyingine hutengwa na wanaume zao na jamii inayowazunguka.

Sanjari na hilo Sullusi alisema kwa mujibu wa Shirika Afya Duniani (WHO) takriban wanawake milioni nne ulimwenguni kote wanaishi na fistula na wengine 50,000 hadi 100,000 wanapata tatizo hilo kila mwaka na wengi wao wanaishi barani Afrika.

Pia alisema kuwa tatizo la Miundombinu mibovu na uhaba wa zahanati hasa vijijini pia ni sababu inayochangia wanawake kutopata huduma za Afya ya uzazi kwa wanawake ambapo hata ushirikiano wa wazazi wenza yaani wanaume juu ya kuwasaidia wake zao wakati wa kujifungua ni mdogo mno.

Sullusi alisema pamoja na hayo asasi hiyo inaandaa kongamano la kuhamasisha wananachi ili kujenga utamaduni wa kwenda katika zahanati na Hospitali kupata elimu ya Afya ya uzazi kuliko hivi sasa ambapo watanzania wengi huanza kupata elimu hiyo wanapopata ujauzito hasa mjini hivyo ameiomba Serikali navyombo vya Habari kuunga mkono jitihada za asasi hiyo kwa ajili ya kupunguza uwezekano wa kutokea Fistula kwa wanawake.

large.jpg
Kushoto ni Mweyekiti wa TACOMO Angelica Sullusi akiwa anajadiliana jambo na Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Gordon Kalulunga mwaka 2011.

TACOMO NI SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI NCHINI TANZANIA


Shirika letu linaitwa Tanzania Community Media Organization (TACOMO).

TUNAPENDA kutoa shukrani zetu za dhati kwa kutupokea katika njia hii ya mawasiliano kupitia mtandao.



TACOMO PROFILE
JINA KAMILI;
Tanzania Community Media Organization.

KIFUPI;
Tacomo.

MWANZILISHI NA KIONGOZI MKUU;
Gordon Frank Kalulunga.

MWAKA WA KUANZA;
2010.

MWAKA WA USAJILI;
Julai 6, 2011.

NAMBA YA USAJILI;
OoNGO/oooo4650

ILIKOSAJILIWA;
Wizara ya jamii jinsia na watoto.

MAHALA TULIPO;
Mbalizi, wilaya ya Mbeya (Vijijini) mkoa wa Mbeya.

LENGO NA MADHUMUNI;
Lengo la shirika ni kusaidia jitihada za serikali katika kuwezesha jamii  katika kuibua na kutatua baadhi ya changamoto za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali zikiwemo za ulinzi wa mtoto, vijana, wazee, jinsia, Afya, Mazingira, Kilimo na kuandaa warsha/ mafunzo, kushiriki na kushirikishwa katika shughuli za kimaendeleo na uwezeshaji kwa vikundi mbalimbali kwa lengo la kutokomeza umasikini.



Aidha tunashiriki na kushirikishwa katika kuunganisha jamii kwa lengo la kutokomeza umasikini na kuibua hoja kisha kuifikishia serikali kupitia vyombo vya habari.

KAZI ZA SHIRIKA;
Moja ya kazi za shirika letu ni kuibua vyanzo vinavyochangia kutokuwa na huduma bora za Afya ikiwemo matatizo ya wanawake, Ulinzi wa watoto ukatili wa kijinsia na kupatanisha jamii zilizofarakana.

MAHALI PA KAZI;
Shirika limesajiliwa kufanya kazi mahala popote Tanzania bara.

MAFANIKIO;
Tangu shirika letu lisajiliwe kisheria, tumeweza kushiriki na kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya kujitolea na vya ujasiliamali ambapo mafanikio makubwa yanaonekana katika kikundi cha usafi na uhifadhi wa mazingira mkoa wa Mbeya kiitwacho Umoja wa Vijana Wazalendo Mbeya (UVIWAMBE), ambacho awali walikuwa wanajitolea lakini kwa sasa wananufaika baada ya kupewa kibali cha kukusanya tozo za usafi katika mji mdogo wa Mbalizi, Halmashauri ya wilaya ya Mbeya.

Aidha tunashirikina vema na Halmashauri ya wilaya ya Mbeya katika kujumuika katika ushawishi wa wananchi kuunda vikundi na ushawishi wa kuchangia maendeleo.

Tumeweza kuwachukua na kuwalipia mafunzo ya uchoraji (Artist) watoto na waliokuwa wa mitaani zaidi ya 10 ambao ni chini ya miaka 17 ambao kwa sasa baadhi wanajitegemea na mmoja bado yupo mafunzoni kwa vitendo kupitia mchoraji Asia Print wa Mbeya kwa michango yetu wenyewe kama wanachama.

Kwa sasa tuna vijana wanne wa mitaani ambao tunawalipia mafunzo ya kuendesha pikipiki (Boda Boda) na kila baada ya miezi mitatu tunatembelea hospitali kuona wagonjwa.


MAWASILIANO YA SHIRIKA
Tanzania Community Media Organization (TACOMO).             
S.L.P 705, Mbeya-Tanzania,
SIMU; 0754 440749/0655 440749/0765 615858


Tunaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa katika kujuzana taarifa mbalimbali za kimaendeleo.