Tuesday 29 March 2016

VIONGOZI WA MTAA WATUHUMIWA UTATA WA FEDHA ZA UMMA

MWENYEKITI wa mtaa wa Nsalala katika Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi, Stephano Mshani na Ofisa mtendaji wa eneo hilo Lwitiko Mwaibindi, wametuhumiwa na wananchi wa eneo hilo kukiuka taratibu za uhifadhi wa fedha zao.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za mtaa huo mwishoni mwa wiki, walisema kuwa, viongozi hao wameuza ardhi ya serikali kisha fedha hizo kuzihifadhi katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti huyo.

Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti huyo alikiri kufanya hivyo na kwamba ardhi hiyo waliuza kiasi cha Milioni Nane.

Baada ya kusema hivyo, ndipo Ofisa Mtendaji wake aliinuka na kulanusha kiasi hicho cha fedha na kwamba Mwenyekiti wake hajawa mwaminifu maana ardhi hiyo waliuza Tsh. 8,650,000.

Ndipo Mwenyekiti aliendelea na kukiri kuwa ni kweli ardhi hiyo iliuzwa kwa kiasi alichokieleza ofisa mtendaji.

Kufuatia utata huo, hali ikabadilika ndipo Diwani wa kata ya Nsalala Kissman Mwangomale, aliinuka na kuwasihi wananchi kuwa watulivu huku akisema kuwa viongozi hao wote ni watuhumiwa na inabidi wakajipange upya.

Alipomaliza kutoa ushauri huo, Mwenyekiti Mshani aliinuka na kuwaambia wananchi kuwa wawape muda na wataleta taarifa ya mapato na matumizi ya fedha hizo ifikapo Aprili mosi mwaka huu na akaahirisha mkutano.

Baada ya kuahirisha mkutano, ikatokea sintofahamu kwa baadhi ya wananchi jinsi mkutano ulivyoairishwa, ndipo Diwani Mwangomale aliwatuliza na kuwaambia kuwa wavute subira mpaka siku ya Ijumaa.

Mwandishi wa habari hii, aliwafuata viongozi hao ofisini ambako walimtaja mnunuzi kuwa ni Gasper Mwamakula (Mtaribani).

"Hizi pesa tulizipokea Machi 17, mwaka huu na nikiwa mimi, Mwenyekiti na mjumbe wetu mmoja tukamteua Mwenyekiti akapeleke pesa hizo kwenye akaunti ya Kijiji lakini baadae akasema ameweka kwenye akaunti yake na kuanza matumizi ndipo nikaandika taarifa kwa Ofisa mtendaji wa kata.kumjulisha na nakala kwa Mkurugenzi" alisema Lwitiko Mwaibindi.

"Hizi pesa ni kweli nilikabidhiwa kupeleka kwenye akaunti ya serikali lakini nilipofika kule nikaambiwa akaunti ipo Domant, ndipo nikarudi na pesa nikawaambia wenzangu wakanikubalia kuweka kwenye akaunti yangu kumbe ulikuwa mtego" alisema Stephano Mshani.

Hata hivyo, imebainika kuwa, tayari fedha hiyo imeanza kutumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya ujenzi wa darasa moja la shule ya msingi Nsalala huku Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi ikiwa haijui chanzo cha fedha hizo ambazo kisheria mali iliyouzwa ilikuwa ni ya Mamlaka na wala si kitongoji.

Vifaa vilivyonunuliwa mpaa sasa kupitia fedha hiyo ambayo Mwenyekiti licha ya kuimiliki kwenye akaunti yake lakini amesema hajui katumia kiasi gani na amebakiwa na kiasi gani ni pamoja na Cement mifuko 60, Nondo 6, Chokaa mifuko 25, misumari, Mchanga trip 3, Madirisha 18, Rangi za ubao lita 3, Bomba za Varanda 3, Milango na flemu zake 3, Bati 7, Shata zamadirisha 36, Mabanzi 12, Kupaka Oil 40,000, Usafiri 50,000, Posho za mafunzi 400,000 na Mbao 900,000.

Baadhi ya mafundi walipoulizwa wamesema kuwa hizo fedha hawajakabidhiwa.

Hata hivyo, jitihada za kujinasua kwa wahusika zinaendelea, ambapo jana juzi Machi 27, mwaka huu, taarifa zimedai kuwa Mwenyekiti wa mtaa huo Stephano Mshani alikutana na mwanasheria wa Halmashauri ya Mbeya, Gasper Msivala na mwanasheria huyo alipoulizwa kwa njia ya maandishi (SMS), alikiri Mwenyekiti huyo kwenda nyumbani kwake na kueleza hali ilivyo huku akiwa mpole na kwamba yeye kamweleza madhara ya alichokifanya na kwamba Mwanasheria hana mipaka ya kutoa ushauri...


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya, Upendo Sanga alipotafutwa ofisini kwake, hakupatikana kwa maelezo ya Katibu muhtasi wake kusema kuwa alikuwa yupo kwenye kikao ofisi za mkoa wa Mbeya.

WANANCHI 78 MBEYA, WAKOSA UMEME TANGU MWAKA 2012

Na Gordon Kalulunga, Mbeya

Wananchi wapatao 78 katika mji mdogo wa Mbalizi jimbo la Mbeya Vijijini mkoani Mbeya, wameshindwa kupatiwa huduma ya umeme tangu walipoomba huduma hiyo mwaka 2012.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi alipotembelea katika eneo hilo shina la Umoja Mtakuja, walisema wana uhitaji wa nishati hiyo lakini mpaka sasa wanasubiri majaliwa na matakwa ya shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Walipoulizwa kama kuna taratibu zozote walizozifanya, walisema tangu mwaka 2012 walijiorodhesha na kupeleka majina yao Tanesco lakini hawajapata jawabu lolote wala kuwaona maafisa wa shirika hilo kupita katika eneo hilo lililopo jirani kabisa na shule ya Sekondari Usongwe ambayo ina umeme.

Mwandishi wa habari hii alifanya jitihada za kuweza kupata majina ya wananchi hao, ambapo alifanikiwa kuyapata majina hayo yakiwa yamesubirishwa katika mafaili ya Tanesco mkoa wa Mbeya.

Majina hayo ni kama yafuatayo;
Boazi Luvanda, Kravery Kazembe, Frank Masinga, John Erasto, Mwanyanje Mwampamba, Issa Mwakifuna, Tosigwe Mwakyusa, Nelbert Mwamwaja, Gimi Ngobile, Ali Ayubu, Maiko Songela, Jasi Mwampashi, Leonard Mwaipopo, Kenneth Simon, Saidi Hayola, Eva Mwakalobo, Pamphili Lema na Paulo Kameta.

Wengine ni Julius Simbeye, Laston Mtafya, Somo Mwakaje, Godwin Sikabenga, Elizabeth Mwalugaja, Waziri Ezekia, Peter Jackson, George mashiwawa, Lazaro Nyusu, Regan Mwankemwa, Gerad Mitingi, William Samson, Geremano Ndelwa, Asajile Godwin, Mlewa Msyani, Aden Kamokene, Mwasomola Mwisivileghe na Tumaini Syonga.

Wananchi wengine waliomo kwenye orodha ya karatasi hiyo ya tangu mwaka 2012 ni Hassan Chaula, Tamali Sampamba, Amani Mwasimba, Felista Josphat, Abdul Ng'elenge, Juma Mwazembe, Aloyce John, Burton Bukuku, Amos Samwel, Tamali Philimon, Gabriel Mtawa, Bahati Ndele na Israel Makobeli.

Wengine ni Maria Mkwela, Gezi Mwashilindi, Jestina Mwalwiji, Hezero Sekeni, Emmanuel Mwandagane, Maiko Yisambi, Justini Francis, Waziri Mwangoka, Luka Kasebele, Edward Mwakyusa, Joseph Kasekwa, Lusajo Boniface na Lusekelo Amenye.

Fadhili Mwashiwawa, Yohana Mbuba, Steven Ngonya, Laison Mwakibinga, Medelina Mwasenga, Mery Pilla, Jackson Halinga, Said Mganga, Sadock Nduka, Sharifu Adson, Mado Godwin, Thobias Mwambona, Paulo Mwewe na Imani Mwaihojo.

Endapo wateja hao wangekubaliwa kupatiwa huduma hiyo ya umeme wa majumbani, kila mmoja angepaswa kulipa kiasi cha Tsh 177,000 ambapo jumla yake ingekuwa Tsh 13,806,000 bila huduma ya nguzo na kila mmoja baada ya kuisha Unit 50 za awali, angepaswa kulipa Tsh. 40,000 ambapo jumla wangelipa 3,120,000 na kila mwezi angelipa Tsh. 10,000 kwa basi shirika hilo lingepata Tsh 780,000 kwa kila mwezi.

Thursday 24 March 2016

MIONGOZO RAHISI YA USIMAMIZI SHIRIKISHI NA UVUNAJI MISITU KATIKA VIJIJI YAZINDULIWA RASMI

Meneja wa kampeni ya Mama Misitu, Gwamaka Mwakyanjala (katikati) akionyesha miongozo hiyo kwa waandishi wa habari, kulia kwake ni Mratibu wa Ukaguzi na Tathmin wa Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Wilbard Mkama na kushoto kwake ni Mratibu Kikundi Kazi Misitu Tanzania, Cassian Sianga.
Balozi wa Kampeni ya Mama Misitu, Asha Salimu alizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa miongozo hiyo.
Mkurugenzi wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF),  Ben Mfungo Sulus akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa miongozo hiyo.

 Wadau wa Misitu wakifuatilia mkutano huo
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo, akizungumza juu ya umuhimu wa wanahabari katika kutoa elimu ya mazingira.
 Picha ya pamoja.
 
 
Kampeni ya Mama Misitu (MMC) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii Machi 23, 2016 imezindua miongozo miwili rahisi ya usimamizi shirikishi wa misitu kwa pamoja na uvunaji katika misitu ya hifadhi ya jamii.

Miongozo hiyo ambayo imetokana na miongozo ya Kiingereza ambayo awali ilichapishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013, inalenga kurahisisha kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya uhifadhi na uvunaji wa rasilimali za misitu kuanzia ngazi za taifa hadi kwa wananchi wenyewe.

Meneja wa kampeni hiyo Gwamaka Mwakyanjala anasema iliwalazimu kuiweka miiongozo hiyo katika lugha rahisi ya Kiswahili ili kuwezesha wananchi kuelewa na kuchukua hatua. 
 
“Miongozo ya awali ilikuwa katika lugha ya kingereza na hivyo kukwaza zoezi la uelimishaji kwa wananchi, tunaamini kwa kutumia miongozi hii iliyo kwenye lugha ya Kiswahili ujumbe utafika kwa walengwa na kampeni yetu itafanikiwa pia” anasema Gwamaka.

Uzindui huo ambao ulifanywa chini ya Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) ulihudhuria na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali na mashirika binafsi.

Kawaida Kampeni ya Mama Misitu (MMC) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii Machi 23, 2016 imezindua miongozo miwili rahisi ya usimamizi shirikishi wa misitu kwa pamoja na uvunaji katika misitu ya hifadhi ya jamii. 
 
Miongozo hiyo ambayo imetokana na miongozo ya Kiingereza ambayo awali ilichapishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013, inalenga kurahisisha kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya uhifadhi na uvunaji wa rasilimali za misitu kuanzia ngazi za taifa hadi kwa wananchi wenyewe. 
 
Meneja wa kampeni hiyo Gwamaka Mwakyanjala anasema iliwalazimu kuiweka miiongozo hiyo katika lugha rahisi ya Kiswahili ili kuwezesha wananchi kuelewa na kuchukua hatua. 
 
“Miongozo ya awali ilikuwa katika lugha ya kingereza na hivyo kukwaza zoezi la uelimishaji kwa wananchi, tunaamini kwa kutumia miongozi hii iliyo kwenye lugha ya Kiswahili ujumbe utafika kwa walengwa na kampeni yetu itafanikiwa pia” anasema Gwamaka. 
 
Uzindui huo ambao ulifanywa chini ya Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF) ulihudhuria na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali na mashirika binafsi. 
 
Chanzo; Maliasili zetu blog.

Monday 7 March 2016

Timu ya Taifa U21 ya Hockey yakabidhiwa bendera

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye katika hafla ya kuiaga Timu ya Taifa ya Magongo U21 kwenda Windhoek, Namibia 
Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 21 (U21) ya mchezo wa magongo imetakiwa kupambana na kurejea na ushindi katika michuano ya vijana barani Afrika inayotarajia kuanza Machi 18 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia.

Akizungumza katika hafla fupi ya kuikabidhi bendera timu hiyo jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana alisema ana imani kubwa kwa vijana hao ambao ni mara yao ya kwanza kufanya vizuri.

Nape alisisitiza, nidhamu watakayoionesha na kujituma katika michuano hiyo itakayotia nanga Machi 28 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia la Vijana Novemba mwaka huu nchini India italitangaza taifa katika mchezo huo na utakuwa mwanzo mzuri.

Kwa upande wao manahodha wa timu hiyo Eliezer Jeremiah na Irene Albert walisisitiza kuwa licha ya kuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki watajitahidi wawezavyo huku wakimsikiliza kocha wao ambaye amewapa mazoezi ya kutosha.

Kocha Valentine Quranta alisisitiza kuwa amekianda kikosi vizuri licha ya kwamba ushindani utakuwa mkubwa sana endapo atapangwa na Ghana, Kenya au Namibia ambao wako vizuri katika mchezo huo.

Pia Ofisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Waziri Barnabas alisisitiza ulazima wa kuisaidia timu hiyo baada ya waziri kuwaomba wafadhili kujitahidi kuingia mikataba ya muda mrefu ili kuweka programu thabiti.

Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Magongo Tanzania (THA), Ibrahim Sykes alisema wanaendelea na juhudi za kuupanua mchezo huo lakini wanakabiliwa na kikwazo cha vifaa suala kwa wizara husika.


Katika hafla hiyo, NMB walitoa shilingi mil. 25 na mabegi ya kusafiria huku Diamond Motors nao wakiunga mkono juhudi za timu hiyo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (katikati) akimkabidhi vifaa Mwenyekiti wa Chama cha Magongo Tanzania Abraham Sykes vilivyotolewa na NMB katika hafla ya kukabidhi bendera ya taifa kwa Timu ya Taifa ya Vijana ya Magongo U21  inayokwenda kushiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika ya Vijana jijini Windhoek, Namibia. (Picha na Jabir Johnson)
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (katikati) akiwa na manahodha wa Timu ya Taifa ya Vijana ya Magongo U21  Eliezer Jeremiah (wa pili kushoto) na Irene Albert (wa pili kulia), katika hafla ya kukabidhi bendera ya taifa kwa timu hiyo inayokwenda kushiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika ya Vijana jijini Windhoek, Namibia.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (kulia) akiwa na Katibu wa THA (kushoto), Mnonda Magani , Kocha Valentine Quranta (katikati) na viongozi wengine wa Timu ya Taifa ya Vijana ya Magongo U21  katika hafla ya kukabidhi bendera ya taifa kwa timu hiyo inayokwenda kushiriki Michuano ya Mataifa ya Afrika ya Vijana jijini Windhoek, Namibia.

Serikali Yaanzisha Mfumo Mpya Wa Malipo Ya Mishahara Kwa Watumishi Wa Umma


SERIKALI imeanzisha mfumo wa Kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana (Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa sekta mbalimbali  katika wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
 
Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa  
 
Waziri Mkuu alisema mfumo huo unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha  taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hadi anapostaafu.

Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, maafisa utumishi walipaswa kukusanya taarifa za watumishi wote walioajiriwa na kuzipeleka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili zikathibitishwe kabla ya kuzipeleka HAZINA kwa maandalizi ya mishahara. 
 
Akitolea mfano wa kada ya ualimu, Waziri Mkuu alisema ajira za walimu zilikuwa zinaanzia Idara ya Utumishi wa Walimu  (TSD)  lakini anapaswa aende kuripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri  (DED) ambaye ni mwajiri wake chini ya TAMISEMI.
 "Hii ilileta ugumu wa malipo ya kupanda madaraja, uhamisho ama likizo kwa sababu mwajiri anakuwa hajatenga hizo fedha."
 
"Sasa hivi tuna Tume ya Utumishi wa Walimu  (TSC) ambayo iko chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kwa hiyo ni rahisi wao kukaa pamoja na kuamua tuwapandishe daraja walimu 10 na wote hao wakalipwa bila bila kuchelewa," alisema.
 
Alisema mfumo huo umeanza kutumika tangu mwaka 2012 na ulianza kwa ajira mpya za walimu na hadi sasa umethibitisha kuwa inawezekana kumlipa mtumishi mshahara wake hata kama ameajiriwa ndani ya mwezi huohuo.
 
"Kama mtumishi anaripoti kwenye kituo kipya hata iwe wilaya ya wapi ili mradi amefika na barua zake zote na ziko sahihi mtu huyu ataingiziwa taarifa zake na wakati huohuo taarifa zitaonekana Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na pia zitapokelewa kwa maafisa wanaoshughikia mishahara kule HAZINA."
 
Alisema changamoto pekee waliyokutana nayo wakati mfumo huo umeanza ilikuwa ni kutoingizwa taarifa za wale ambao wameripoti baada ya tarehe 10 ya mwezi husika. 
"Hii ni kwa sababu matayarisho ya mishahara yanakuwa yameshaanza. Kwa hiyo wengi walishauriwa kuripoti kati ya tarehe 25 hadi tarehe 9 ya mwezi uliofuata na wote hawa hawakupata matatizo ya kucheleweshewa mshahara," alisema.
 
Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema  Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya. 
"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara  na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua hiyo hiyo " alisema

AKATISHA ZIARA KUTOKANA NA MSIBA
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelazimika kukatisha ziara ya mkoa wa Simiyu ambayo ilikuwa imalizike kesho kutokana na msiba wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambayo alipangiwa kuitembelea leo.
 
Mkurugenzi huyo Bw. Traceas Kagenzi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kutokana na shinikizo la damu. Atasafirishwa kwenda Muleba  kwa mazishi.

Akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya kumuombea marehemu Kagenzi iliyofanyika nyumbani kwake Maswa mjini, Waziri Mkuu alisema ameshtushwa na msiba huo uliotokea ghafla na kwamba Taifa limempoteza mtumishi mahiri ambaye bado Taifa lilikuwa likimtegemea.

"Nimeshtushwa sana na taarifa za msiba huu. Nimeambiwa hadi juzi usiku alikuwa akishirikiana na Mkuu wa Wilaya hii kuandika taarifa ya ziara ya wilaya hii. Kwa niaba ya Serikali, ninawapa pole sana wafiwa na Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi," alisema.

"Nimelazimika kukatisha ziara ya mkoa huu kwa sababu huyu ni mtumishi mwenzetu" alisema Waziri Mkuu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 6, 2016.