Saturday 14 November 2015

Dawa za kulevya zaleta uchugu kwa vichanga na wajawazito Tanzania



NA GORDON KALULUNGA.

DAWA za kulevya ni kemikali za majimaji, majani au unga wenye kemikali zenye vilevya, ambazo zikitumiwa na viumbe, hubadili hisia, fikra na tabia ya mtumiaji, akiwemo binadamu na viumbe vingine.

Zinaweza zikawa halali au si halali, asili au zinazotengenezwa kiwandani, katika mfumo wa vidonge, unga au maji, zikatumika kwa njia ya kujidunga, kunusa, kula, kunywa, kuvuta, au kupiga bamba.

Dawa hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo yanatenganishwa kutokana na jinsi dawa hizo zinavyoathiri mfumo wa utendaji kisaikolojia (psychoactive substance).

Makundi hayo ni Vichangamshi (Stimulants) mfano; cocaine, tumbaku na khat.


Kundi la pili ni Vipumbaza (Depressants), mfano; pombe, heroine, methadone, codeine, morphine, na gundi.

Kundi la tatu ni Vileta Njozi (Hallucinogens). Mfano ; uyoga, bangi.

Wanawake wajidunga waeleza yaliyowapata wakati wa ujauzito.
Baadhi ya wanawake wanaotumia dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam, na walioacha kutumia, wanaeleza adha na changamoto wanazozipata katika maisha yao ndani ya jamii.

Wanasema, walijitumbukiza katika matumizi ya dawa hizo bila kujua kuwa ni utumwa na ugonjwa mbaya.

Fatuma Athuman, mama wa mtoto mmoja wa kike, anasema alianza kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin kwa kuchanganya na sigara huku akivuta, kisha akaanza kujidunga na sindano na hatimaye Baba yake akamfukuza nyumbani, akaenda mitaani ambako pia alikuwa akiambulia mateso ya polisi ya kukamatwa na kupigwa.

“Mwaka 2012 ndipo nilipotamani kuacha kutumia dawa za kulevya, nikajipeleka kwenye tiba ya Methadone inayopatikana Mwananyamala, Temeke na Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, kwa sasa naendelea vizuri”anasema Fatuma Athuman.


Fatuma Side(31), anasema alianza kutumia bangi akiwa na miaka 25, na hakuwa na mtoto, baadaye akaaza kutumia Cocain na sasa ana mtoto.

“Nilipata mimba nikiwa nyumbani, lakini kipindi hicho nilikuwa nashinda sana maskani kuvuta. Nilipojifungua nikaendelea kwenda na mtoto huko maskani, lakini ikanishangaza mtoto alipoanza kupata akili, akawa anaiga vitendo vyote tulivyokuwa tukifanya maskani…, nikaanza kumwacha nyumbani kwa wazazi wangu ili asiharibike”anasema Fatuma Side.

Anasema katika maisha yake ya utumizi wa dawa za kulevya, anakumbuka kuwa aliuza vitu vyake vya ndani ili ajipatie pesa kwa ajili ya  kununua dawa za kulevya!

Wajawazito na ulalaji katika maskani za kuvutia dawa za kulevya
Fatuma anasema, ulalaji wa wanawake wenye mimba na watoto huko  maskani siyo mzuri, mwanamke mmoja analala katikati ya wanaume kumi, huku mtoto akiwa anapigwa na baridi kwa sababu siku nyingine usiku kunakuwa na baridi kali, huku wengine wakiendelea kuvuta bangi na wengine wakijidunga.

“Ukiwa na mtoto mdogo maskani ni shida sana, unalala mwanamke peke yako katikati ya wanaume kumi huku mtoto mchanga akipigwa na baridi, unaamka asubuhi mama mtu miguu ikiwa imevimba na wakati huo huo utakuta umelala saa nane usiku baada ya kutoka labda stereo au Muhimbili kutafuta unga” anasema Fatuma Side.


Anaeleza kuwa amewahi kukamatwa na askari polisi na kupelekwa gereza la segerea kwa siku ishirini, ambako anasema maisha ya huko hayana utu kabisa, kisha siku ya ishirini alipopelekwa mahakamani akaachiwa huru.

Anasema, mtumiaji wa dawa za kulevya ana hatari ya kupata maambukizi ya VVU na homa ya ini B na C, kutokana na ngono na udungaji usio salama ambao unasababishwa na matumizi ya kuchangia sindano za kujidungia na kwamba uzoefu wake mpaka sasa wengi wa wajidunga wana maambukizi ya VVU na kifua kikuu kutokana na tabia za kulundikana kulala na kufanya ngono zisizo salama na baadhi ya wanawake kufanya biashara ya ngono isiyo salama.

Kwa sasa anasema ameacha kutumia dawa za kulevya, kutokana na msaada na huduma anazozipata kutoka shirika la Medecins du Monde (MDM), na anaishi kwenye nyumba yake aliyojenga, bado hajaolewa, wadogo zake na wazazi wakimuona hawalii tena, jamii inamuheshimu si kama zamani.

Kwa sasa nimwelimishaji rika wa MdM na ana wahudumia wenzake kwa kuwapa elimu ya afya, kondomu na vifaa salama vya kujidungia hasa ambao wanaendelea kutumia dawa za kulevya na anasema wengi wanabadilika ikiwemo kupunguza matumizi na kuacha kabisa kama yeye.

Mbali na huyo, Salima Hamad (30), anasema yeye amevuta bangi kwa kuchanganya na heroin kwa miaka 14, na amejidunga kwa muda wa miaka 5.

Anasema “nilipo anza kutumia dawa za kulevya, mwanzoni hakuna aliyegundua, siku zilivyokwenda nilianza kudhoofika kiafya, mama aliambiwa kuwa mwanao anatumia dawa za kulevya, aliponiuliza, nikamkatalia lakini siku zilivyokwenda afya yangu ilianza kudhoofika, nyumbani walithibitisha kuwa natumia dawa za kulevya walikuwa wakinisema sana, nikaondoka nyumbani,”anasema Salima.

Anasema katika maisha ya utumiaji wake, alinyanyapaliwa, kila alipokuwa akipita hasa maeneo ambayo wanamfahamu alikuwa anasemwa vibaya kwa dharau kuwa siku hizi ni mwizi, mtu yeyote asimuamini.

“Niliumia sana, kwani hakuna mtu aliyekuwa akiniamini, kwani jamii ishakuwa na mtazamo kuwa kila mtumiaji wa dawa za kulevya ni mwizi”.anasema.

Yeye akiwa mwanamke mtumiaji wa dawa za kulevya, alipokuwa mjamzito kwa mara ya kwanza hakuwahi kwenda kliniki kwa sababu ya hofu ya kuwaeleza wahudumu jinsi gani wangeweza kumwelewa wakati hakuwa na fedha.

“Kwa muonekano wangu, nilijipa majibu kuwa nesi hawezi kunijali, kwahiyo niliendelea na maisha ya maskani mpaka nikajifungulia huko huko, sikuwa na chakula cha mtoto, hivyo hivyo nikipata haya, nikikosa sawa, huku nilikuwa nikiendelea kutumia dawa za kulevya” anasema Salima.
Alipoulizwa kuwa nani alimsaidia wakati wa kujifungua, anasema ni wenzake. 

Dr. Moke Magoma wa shirika la Evidence For Action(E4A) linaloshughulika na mradi wa kuokoa maisha ya mama na mtoto nchini(Mama Ye!), ambaye ni mbobevu wa masuala ya afya ya uzazi, anasema robo tatu ya wajawazito wanaobeba mimba na kujifungua, wanajifungua salama bila hata wasaidizi wenye ujuzi bali robo inayobaki ndiyo wanapata shida na baadhi kufariki.

“Bahati mbaya ni vigumu kuwatambua wale robo kwasababu matatizo hutokea ghafla na bila kutegemewa hivyo haja ya akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya afya vyenye wataalam wenye ujuzi wa ukunga ni muhimu ingawa bahati mbaya bado kuna vituo hasa vijijini havina wataalam maana siyo kila mhudumu ni mkunga” anasema Dr. Moke Magoma.

Katika ujauzito wake wa pili, Salima anaeleza kuwa akafahamu kuwa kuna shirika la MdM linalosaidia wajidunga, alikwenda huko na akahudumiwa kama mtoto, akapelekwa hospital, akapatiwa vifaa vya kujifungulia na akawa anafuatiliwa mpaka akajifungua huku akipatiwa pia unga wa uji na chakula cha kwake na mtoto.

Kwa sasa anasema anatumia dawa aina ya methadone, inayosaidia kupunguza kiasi cha matumizi ya dawa za kulevya na kuacha, anasema amebadilika hata mwili wake, anaenda kwenye kituo cha MdM kupatiwa elimu na kupimwa kuangalia hali yake ya maambukizi.

“Kwa ufupi kutokana na mradi huu tunaonekana sasa watu, hata nikienda nyumbani wanaongea na mimi kama mtu mwingine”anasema. 

Mtaalam wa mifumo ya kompyuta katika Tume ya uratibu na udhibiti dawa za kulevya Tanzania bara, January Ntisi, (DCC), anasema matumizi ya dawa za kulevya nchini yanasababishwa na sababu tofauti ikiwemo makundi rika, unyanyasaji wa kisaikolojia wanaofanyiwa watu, upungufu wa maadili mema, ushawishi, kuonesha ufahari na mambo mengi.

Anasema, urefu wa ukanda wa bahari wenye vipenyo vingi ni moja ya sababu ya dawa hizo kuendelea kuingia nchini.

Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa, mazingira ya bandari ya Zanzibar ni tatizo katika kufanikisha kupunguza uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya kutokana na bandari hiyo kuwa wazi kiasi ambacho mtu yeyote anaweza kuingiza kitu chochote nchini mbali na dawa za kulevya.

Ofisi ya kamanda wa polisi Mkoa wa Unguja Zanzibar, inakiri kuwa, uingizaji wa boti zaidi ya moja kwa wakati mmoja bandarini ni moja ya kikwazo katika kupambana na wahalifu na kwamba mazingira ya Kijiografia ya visiwa vya Zanzibar yanachangia kwasababu kuna zaidi ya bandari 500 za kienyeji Unguja pekee, ambazo zinaweza kuingiza madawa ya kulevya kwa kutumia vyombo vidogo vidogo vya kienyeji wakati wowote ule wapendao, na kwa sababu Polisi haina vyombo vyovyote vya kufanyia doria ni vigumu kufika maeneo kama hayo ambayo kwa hakika yanatakiwa uangalizi wa mara kwa mara. 

Watumishi wa MDM waeleza huduma waitoayo
Mfanyakazi (Outreach Worker) wa shirika la Medecins du Monde(MdM) la wilayani Temeke, Aina Mrope, anasema anaumia kuwaona wanawake wanaotumia dawa za kulevya huku wakiwa na familia.

“Tunawaendea hata majumbani na kuwasaidia kuwapa elimu ya afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka hospitali wale wanaoumwa na kuwapatia kondomu wale ambao wanafanya biashara ya ngono”anasema Aina.

Anasema wanawake wanaotumia dawa hizo za kulevya na kuhudumiwa na kituo chao, wanapatiwa pia pamba, nguo, chakula, dawa za nywele, mafuta, vipodozi na kila siku kuu wanapatiwa mavazi.

Mshauri wa masuala ya saikolojia wa shirika hilo la MDM, Benjamin Myovela, anasema moja ya kazi zinazofanywa na kitengo chake ni kuwashauri watumiaji madhara ya udungaji usio salama na hatari zake, ambapo jambo la kuamua kuacha au kuendelea ni la muhusika mwenyewe, lakini akiwa bado anatumia atumie kwa njia ya usalama ili asipate maambukizi ya VVU na homa ya ini B na C au matatizo mengine ya kiafya. 
Mshauri wa masuala ya afya wa shirika hilo, Prof. Joseph Mbatia, anasema kuwa kundi la wanaotumia dawa za kulevya lipo katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU.

Anasema kundi hilo likiachwa bila kupewa elimu na kusaidiwa katika matibabu na kujikinga, jamii itakuwa kwenye hatari zaidi kwasababu kuna baadhi wanafanya biashara ya ngono.


“Kuna wanawake wanaotumia dawa za kulevya na kufanya biashara ya ngono kwa lengo la kupata fedha, wanakutana na watu ambao hawatumii ambao pia endapo mwanamke huyo ana maambukizi, jamii nzima inakuwa hatarini” anasema Prof. Mbatia.

Meneja wa mafunzo wa shirika hilo, Damali Lucas, anasema“matatizo kwa wanawake wanaoutumia dawa za kulevya ni mengi sana, muda mwingi jamii inawalaumu na kuona kuwa maisha wanayoishi wanajitakia au wamependa.


“Kama jamii hatukumbuki kuwa kuna wengine wameingia katika matumizi ya dawa za kulevya kwa ushawishi kutoka kwa wapenzi wao, wamefiwa wazazi wao, kwa hiyo hawakuwa na uangalizi mzuri.” Anasema Damali.

Anasema, wanawake wanaotumia dawa za kulevya wanakumbwa na matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa kupigwa hasa na wapenzi au hata watu kutoka kwenye jamii, wanachukuliwa kama wamama ambao hawawezi kulea watoto, kuna wengine wakijifungua watoto wananyang’anywa kwa madai hawawezi kulea.


“Kwa sasa MdM inajitahidi sana kuwafikia wanawake wanaotumia dawa za kulevya popote walipo majumbani kwao na kituoni kwa sababu kutokana na utafiti uliofanyika kiwango cha maambukizi ya VVU kwa wanawake wanaotumia dawa za kulevya kipo zaidi ya asilimia 60%, kwa hiyo ni hatari sana kwa afya ya jamii kwasababu wanaingiliana na watu wa kawaida hata kwenye masuala ya kingono” anasema Damali.


Pia anasema MdM inatoa huduma za kisheria kwa wanawake wajidunga na walioacha kutumia dawa za kuelvya, huduma za afya ya uzazi, tiba na ushauri wa kisaikolojia ili wawe na afya bora na kuheshimika kama wanawake wengine.

Taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini ya mwaka 2011, iliyotolewa na tume ya kuratibu udhibiti wa dawa za kulevya, chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya kuzuia biashara haramu ya dawa za Kulevya [Sura ya 95], inaonesha kuwa, dawa za kulevya zinazotumiwa kwa wingi nchini ni bangi ikifuatiwa na mirungi, heroin na cocaine.

Dawa nyingine ni kama vile gundi na petrolpamoja na dawa za tiba zenye madhara ya kulevya zikiwemo valium, morphine na napethidine.

Inasema kuwa, matumizi ya dawa hizi yamejikita zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa na Morogoro ambapo wengi wa watumiaji ni vijana wa kiume wenye umri kati ya miaka 12-35.

Taarifa hiyo inasema kuwa, matumizi haya hufanyika kwa siri katika maeneo mbalimbali yakiwemo makaburini, mageto, majengo yasiyokamilika, magofu, vijiweni na viwanja vya michezo.


Makala hii imeandikwa kwa msaada wa mfuko wa vyombo vya habari Tanzania(TMF), Tume ya kuratibu udhibiti wa Dawa za kulevya nchini(DCC) na Dawati la Umoja wa Mataifa la kupambana na mihadarati na uhalifu (UNODC).

Mwandishi wa makala 0754 440749
Email; kalulunga2006@gmail.com

No comments:

Post a Comment