Saturday 14 November 2015

FISTULA YATESA WANAWAKE MBEYA.

Mkurugenzi wa Shirika hilo Gordon Kalulunga (kushoto).

Mbeya Vijijini na Mbozi vinara ugonjwa wa Fistula.

  • Serikali itoe elimu na kuwatibu wagonjwa.
  • Mwanamke mmoja ang’olewa kizazi.

ASASI isiyokuwa ya Kiserikali ya Tanzania Community Media Organization (TACOMO) yenye makao makuu mkoani Mbeya, imesema ugonjwa wa matundu sehemu za siri kwa wanawake (Fistula) umekuwa mkubwa mkoani humo hivyo Serikali inatakiwa kuvalia njuga ugonjwa huo unaotibika.

Wakizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya, viongozi wa asasi hiyo wamesema asasi yao imefanya uchunguzi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na kubaini maeneo yenye wagonjwa wengi wa Fistula ikiwemo wilaya ya Mbeya Vijijini na Mbozi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Gordon Kalulunga alisema katika wilaya hizo baadhi ya maeneo ndiyo ulikotopea(komaa) ugonjwa huo na wanawake wengi wanashindwa kujitokeza kutibiwa ugonjwa huo kutokana na elimu duni ya matibabu ya ugonjwa huo ambao matibabu yake yanatolewa bure na Serikali.

Kalulunga alizitaja wilaya za Mbozi na Mbeya Vijijini kuwa ni wilaya za mkoa wa Mbeya zenye wagonjwa wanawake wengi walioathiriwa na ugonjwa huo wa Fistula hivyo Serikali kupitia Wizara ya Afya inapaswa kuchukua hatua za makusudi kuwarejeshea utu wanawake wenye matatizo hayo ya Fistula kwa kuanzisha kampeni yenye tija kwa kushirikiana na Hospitali teule ya Ifisi na Hospitali ya Rufa ya Mbeya kitenmgo cha wazazi Meta.

Aidha alisema mbali na kushirikiana na Hospitali hizo pia Serikali iongeze wataalam katika Hospitali hizo wenye uwezo wa kutibu Fistula tofauti na sasa ambapo Hospitali hizo zina Mganga mmoja mmoja wenye uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

‘’Tumefanya uchunguzi wa muda mrefu tangu mwezi Mei mwaka 2010 na kubaini kuwa wanawake wengi katika wilaya hizo wana Fistula lakini hawajajitokeza kutibiwa kwa kuogopa na wanatengwa katika shughuli za kijamii na baadhi wamekimbiwa na waume zao hivyo tunaiomba Serikali ichukue Jitihada za makusudi kuanzisha kampeni za kuwasaidia wanawake hao zitakazopelekea kupata matibabu na ikiwezekana matangazo yatengenezwe na Haki Elimu’’ alisema Kalulunga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa asasi hiyo Angelica Sullusi alisema ugonjwa huo hutokana na jeraha wanalopata kina mama wakati wa kujifungua baada ya kupata uchungu kwa muda mrefu na pia kuwa na njia ndogo ya uzazi kiasi kwamba kichwa cha mtoto kinashindwa kupita kwa usalama wakati wa kujifungua.

Mgandamizo huo wa mtoto husababisha tundu katika njia ya uzazi na kibofu cha mkojo na mara nyingine katika njia ya haja kubwa na kusababisha muathirika kutoka na haja hizo bila ya mpangilio au kujizuia.

Kutoka huko na haja ovyo, huacha unyevunyevu mwingi katika sehemu za siri na kusababisha harufu mbaya. Wengi wenye tatizo hili hulazimika kuishi kwa hali ya aibu na mara nyingine hutengwa na wanaume zao na jamii inayowazunguka.

Sanjari na hilo Sullusi alisema kwa mujibu wa Shirika Afya Duniani (WHO) takriban wanawake milioni nne ulimwenguni kote wanaishi na fistula na wengine 50,000 hadi 100,000 wanapata tatizo hilo kila mwaka na wengi wao wanaishi barani Afrika.

Pia alisema kuwa tatizo la Miundombinu mibovu na uhaba wa zahanati hasa vijijini pia ni sababu inayochangia wanawake kutopata huduma za Afya ya uzazi kwa wanawake ambapo hata ushirikiano wa wazazi wenza yaani wanaume juu ya kuwasaidia wake zao wakati wa kujifungua ni mdogo mno.

Sullusi alisema pamoja na hayo asasi hiyo inaandaa kongamano la kuhamasisha wananachi ili kujenga utamaduni wa kwenda katika zahanati na Hospitali kupata elimu ya Afya ya uzazi kuliko hivi sasa ambapo watanzania wengi huanza kupata elimu hiyo wanapopata ujauzito hasa mjini hivyo ameiomba Serikali navyombo vya Habari kuunga mkono jitihada za asasi hiyo kwa ajili ya kupunguza uwezekano wa kutokea Fistula kwa wanawake.

large.jpg
Kushoto ni Mweyekiti wa TACOMO Angelica Sullusi akiwa anajadiliana jambo na Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo Gordon Kalulunga mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment