Tuesday 29 March 2016

VIONGOZI WA MTAA WATUHUMIWA UTATA WA FEDHA ZA UMMA

MWENYEKITI wa mtaa wa Nsalala katika Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi, Stephano Mshani na Ofisa mtendaji wa eneo hilo Lwitiko Mwaibindi, wametuhumiwa na wananchi wa eneo hilo kukiuka taratibu za uhifadhi wa fedha zao.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za mtaa huo mwishoni mwa wiki, walisema kuwa, viongozi hao wameuza ardhi ya serikali kisha fedha hizo kuzihifadhi katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti huyo.

Akijibu tuhuma hizo, Mwenyekiti huyo alikiri kufanya hivyo na kwamba ardhi hiyo waliuza kiasi cha Milioni Nane.

Baada ya kusema hivyo, ndipo Ofisa Mtendaji wake aliinuka na kulanusha kiasi hicho cha fedha na kwamba Mwenyekiti wake hajawa mwaminifu maana ardhi hiyo waliuza Tsh. 8,650,000.

Ndipo Mwenyekiti aliendelea na kukiri kuwa ni kweli ardhi hiyo iliuzwa kwa kiasi alichokieleza ofisa mtendaji.

Kufuatia utata huo, hali ikabadilika ndipo Diwani wa kata ya Nsalala Kissman Mwangomale, aliinuka na kuwasihi wananchi kuwa watulivu huku akisema kuwa viongozi hao wote ni watuhumiwa na inabidi wakajipange upya.

Alipomaliza kutoa ushauri huo, Mwenyekiti Mshani aliinuka na kuwaambia wananchi kuwa wawape muda na wataleta taarifa ya mapato na matumizi ya fedha hizo ifikapo Aprili mosi mwaka huu na akaahirisha mkutano.

Baada ya kuahirisha mkutano, ikatokea sintofahamu kwa baadhi ya wananchi jinsi mkutano ulivyoairishwa, ndipo Diwani Mwangomale aliwatuliza na kuwaambia kuwa wavute subira mpaka siku ya Ijumaa.

Mwandishi wa habari hii, aliwafuata viongozi hao ofisini ambako walimtaja mnunuzi kuwa ni Gasper Mwamakula (Mtaribani).

"Hizi pesa tulizipokea Machi 17, mwaka huu na nikiwa mimi, Mwenyekiti na mjumbe wetu mmoja tukamteua Mwenyekiti akapeleke pesa hizo kwenye akaunti ya Kijiji lakini baadae akasema ameweka kwenye akaunti yake na kuanza matumizi ndipo nikaandika taarifa kwa Ofisa mtendaji wa kata.kumjulisha na nakala kwa Mkurugenzi" alisema Lwitiko Mwaibindi.

"Hizi pesa ni kweli nilikabidhiwa kupeleka kwenye akaunti ya serikali lakini nilipofika kule nikaambiwa akaunti ipo Domant, ndipo nikarudi na pesa nikawaambia wenzangu wakanikubalia kuweka kwenye akaunti yangu kumbe ulikuwa mtego" alisema Stephano Mshani.

Hata hivyo, imebainika kuwa, tayari fedha hiyo imeanza kutumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya ujenzi wa darasa moja la shule ya msingi Nsalala huku Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi ikiwa haijui chanzo cha fedha hizo ambazo kisheria mali iliyouzwa ilikuwa ni ya Mamlaka na wala si kitongoji.

Vifaa vilivyonunuliwa mpaa sasa kupitia fedha hiyo ambayo Mwenyekiti licha ya kuimiliki kwenye akaunti yake lakini amesema hajui katumia kiasi gani na amebakiwa na kiasi gani ni pamoja na Cement mifuko 60, Nondo 6, Chokaa mifuko 25, misumari, Mchanga trip 3, Madirisha 18, Rangi za ubao lita 3, Bomba za Varanda 3, Milango na flemu zake 3, Bati 7, Shata zamadirisha 36, Mabanzi 12, Kupaka Oil 40,000, Usafiri 50,000, Posho za mafunzi 400,000 na Mbao 900,000.

Baadhi ya mafundi walipoulizwa wamesema kuwa hizo fedha hawajakabidhiwa.

Hata hivyo, jitihada za kujinasua kwa wahusika zinaendelea, ambapo jana juzi Machi 27, mwaka huu, taarifa zimedai kuwa Mwenyekiti wa mtaa huo Stephano Mshani alikutana na mwanasheria wa Halmashauri ya Mbeya, Gasper Msivala na mwanasheria huyo alipoulizwa kwa njia ya maandishi (SMS), alikiri Mwenyekiti huyo kwenda nyumbani kwake na kueleza hali ilivyo huku akiwa mpole na kwamba yeye kamweleza madhara ya alichokifanya na kwamba Mwanasheria hana mipaka ya kutoa ushauri...


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya, Upendo Sanga alipotafutwa ofisini kwake, hakupatikana kwa maelezo ya Katibu muhtasi wake kusema kuwa alikuwa yupo kwenye kikao ofisi za mkoa wa Mbeya.

No comments:

Post a Comment