Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye katika hafla ya kuiaga Timu ya Taifa ya Magongo U21 kwenda Windhoek, Namibia |
Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 21 (U21) ya mchezo wa magongo
imetakiwa kupambana na kurejea na ushindi katika michuano ya vijana barani
Afrika inayotarajia kuanza Machi 18 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuikabidhi bendera timu hiyo jana,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ofisini kwake jijini
Dar es Salaam jana alisema ana imani kubwa kwa vijana hao ambao ni mara yao ya
kwanza kufanya vizuri.
Nape alisisitiza, nidhamu watakayoionesha na kujituma katika michuano
hiyo itakayotia nanga Machi 28 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kufuzu kucheza
Kombe la Dunia la Vijana Novemba mwaka huu nchini India italitangaza taifa
katika mchezo huo na utakuwa mwanzo mzuri.
Kwa upande wao manahodha wa timu hiyo Eliezer Jeremiah na Irene Albert
walisisitiza kuwa licha ya kuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki watajitahidi
wawezavyo huku wakimsikiliza kocha wao ambaye amewapa mazoezi ya kutosha.
Kocha Valentine Quranta alisisitiza kuwa amekianda kikosi vizuri licha
ya kwamba ushindani utakuwa mkubwa sana endapo atapangwa na Ghana, Kenya au
Namibia ambao wako vizuri katika mchezo huo.
Pia Ofisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Waziri Barnabas alisisitiza ulazima wa
kuisaidia timu hiyo baada ya waziri kuwaomba wafadhili kujitahidi kuingia
mikataba ya muda mrefu ili kuweka programu thabiti.
Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Magongo Tanzania (THA), Ibrahim Sykes
alisema wanaendelea na juhudi za kuupanua mchezo huo lakini wanakabiliwa na
kikwazo cha vifaa suala kwa wizara husika.
Katika hafla hiyo, NMB walitoa shilingi mil. 25 na mabegi ya kusafiria
huku Diamond Motors nao wakiunga mkono juhudi za timu hiyo.
No comments:
Post a Comment