Monday 4 July 2016

Shisha yapigwa marufuku Tanzania, hakuna kuvuta sigara hadharani Dar


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, jana amemaliza kazi. Amepiga marufuku matumizi ya ulevi aina ya Shisha nchini ambao umesambaa kwa vijana wengi pamoja na watu wazima.

Marufuku yake imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kupiga marufuku matumizi ya kilevi hicho pamoja na uvutaji wa sigara hadharani mkoani humo.

Wengi, hata ambao hawakuwahi kutumia sigara maishani mwao, walikuwa wamekimbilia uvutaji wa Shisha kwa kujidanganya kwamba kilevi hicho ambacho nacho kinavutwa, hakina madhara kama sigara.

Wanawake kwa wanaume wanavuta Shisha, wengine hadharani, na huona fahari wanapojisikia kulewa huku wakijifariji kwamba hawawezi upata madhara.

Lakini marufuku ya Waziri Mkuu imemaliza kazi, kwa sababu hivi sasa kilevi hicho kimeharamishwa na hakina tofauti na dawa za kulevya.

Katazo la uvutaji wa sigara hadharani limewakumba wengi, kwani si mmoja au wawili wanaotumia sigara, jambo kuwa ni hatari kwa afya za watumiaji.

Mei 31 ya kila mwaka, ni siku ya maadhimisho ya siku ya kutotumia tumbaku duniani kote lakini bado inaonekana matatizo ya matumizi ya tumbaku na uvutaji sigara yanaongezeka kwa kasi kubwa katika jamii, huku madhara yake yakiwa makubwa ikiwemo maradhi ya kifua kikuu.

Licha ya ukweli kwamba, uvutaji wa sigara ni aina mojawapo ya uvurugaji wa ustaarabu kwa wasiotumia bidhaa hizo, sheria ya nchi inapiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani huku suala la kiafya likipewa kipaumbele.

Fikra Pevu imekuwa ikiandika mara kwa mara kuhusu matumizi na madhara ya uvutaji wa sigara kiafya, japo kampuni zinazohusika na shughuli za uzalishaji na utengenezaji zinaiingizia nchi mapato makubwa.

Mnamo mwaka 2003, Bunge la Tanzania lilipitisha sheria inayokataza matumizi ya sigara hadharani, huku ikilenga kukomesha madhara ya kiafya kwa wavutaji wenyewe na wale wanaoathirika kupitia kuvuta moshi wa sigara kutoka kwa wavutaji.

Haya yameelezwa na kufafanuliwa vyema katika Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL, ya mwaka 2003, Kipengele cha 12(1).

‘Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako’, tahadhari ambayo imebandikwa kwenye pakti za sigara, umekuwa kama wimbo uliozoeleka masikioni mwa watu kuhusu kujulishwa madhara ya sigara, lakini wanapuuzia huku wakihoji kuhusu uwepo wa madhara na wakati huo huo viwanda vinapatiwa vibali vya kufanya biashara hizo za uzalishaji na wakulima wanaendelea kuhimizwa kuongeza uzalishaji.

Kutokana na sheria hiyo kuwepo, japokuwa imekuwa kimya sana ikiwapa mwanya watu kuwa huru kuvuta sigara kwa jinsi wanavyohitaji, imemlazimu Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kutoa tamko juu ya jambo hilo.

Tamko hilo la kupiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani, linakuja sambamba na zuio la utumiaji wa shisha pamoja na vitendo vya ushoga vilivyoonekana kushika kasi nchini, huku vikipewa kipaumbele cha kuongelewa hata katika vyombo vya habari.

Makonda amewataka wakuu wapya wa wilaya katika mkoa wake kulifanyia kazi jambo hilo na kuwakamata wale wote ambao watabainika wakivuta sigara, shisha na wanaoushabikia ushoga na kuunga mkono kwa kutoa misaada kupitia NGOs.

Katika matoleo yaliyopita Fikra Pevu ilieleza baadhi ya madhara ya matumizi ya sigara na tumbaku, ilipoitaja nchi ya China kuwa na idadi kubwa ya watu Zaidi ya milioni moja wanaokufa kutokana na magonjwa yanayotokana na uvutaji wa sigara na matumizi mengine ya tumbaku.

Aidha, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2003, zinaonyesha kuwa kila baada ya sekunde 10, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na maradhi yatokanayo na matumizi ya tumbaku.

Takwimu kutoka (WHO) 2003, zilionyesha kuwa, inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2025, vifo vitakavyotokana na matumizi ya tumbaku vitaongezeka kwa kiwango cha asilimia 70 kuliko ilivyokuwa mwaka 2003.

Pia takwimu hizo zinaonyesha kuwa kufikia mwaka 2030, idadi ya watu milioni 10 watakuwa wakifariki dunia kila mwaka kutokana na uvutaji wa sigara ulimwenguni, huku ikitajwa kuwa asilimia 70 ya vifo hivyo vikitoka katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwemo.

Wataalamu wa afya wanayataja magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababishwa na matumizi ya tumbaku au sigara kuwa ni; saratani ya ngozi, saratani ya mapafu, saratani ya kizazi, saratani ya koo, saratani ya kinywa, saratani ya kibofu, matatizo katika mfumo wa upumuaji, udhaifu katika mifupa (Osteoporosis), kuwahi kumaliza kufikia mzunguko wa hedhi kwa wanawake kabla ya muda wa ukomo, athari kwa wajawazito (kuzaa mtoto njiti), kupungukiwa na vitamin mwilini pamoja na kupungua kwa nguvu za kiume au kike.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba, madhara ya hewa ya tumbaku na sigara si kwa wanadamu pekee, bali hata wanyama na mimea vinaathirika kutokana na moshi huo kwani usambaa kwa haraka kufika mbali kitu ambacho huwezi kugundua kwa njia ya kawaida isipokuwa vipimo maalum vya hewa.

Mwaka 1993, Shirika la Kulinda Mazingira la Marekani (EPA) lilitoa taarifa kukadiria kwamba zaidi ya wanyama 3,000 ikiwemo mimea hupoteza maisha kila mwaka, kutokana na kupokea hewa ya sigara au tumbaku.

Kuvuta moshi unaotokana na mtu mwingine au vitu vingine ambao siyo moja kwa moja, ni hali mojawapo ya uvutaji wa sigara, ambayo madhara yake ni sawa na yule mtu anayevuta moja kwa moja, pia husababisha magonjwa, hivyo basi tamko la mkuu wa mkoa kuzuia uvutaji hadharani utasaidia kupunguza madhara ya kiafya, inabidi liwe mfano kwa mikoa mingine kote nchini ikiwa ni utekelezaji na kuimarisha afya za Watanzania.’

No comments:

Post a Comment